SERIKALI YAZINDUA KIPINDI CHA MCHEZO WA RADIO KUHUSU UMUHIMU WA USHIRIKISHWAJI WANAWAKE NA VIJANA KATIKA KUKUZA SEKTA YA KILIMO.
SERIKALI imesema sekta ya kilimo inaendelea kuwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa asilimia 25% ya pato la taifa na kuajiri asilimia 75% ya watanzania wakiwemo wanawake na vijana.
Hayo
yamesemwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Richard Kasuga wakati wa uzinduzi wa mchezo wa
redio uitwao KUMEKUCHA unaotarajia kuonyesha mchango wa wanawake na vijana
katika kutokomeza tatizo la uhaba wa chakula nchini.
Kasuga
amesema kuwa igizo hilo la mchezo wa redio, litaakisi umuhimu wa ushirikishwaji
wa wanawake na vijana katika kukuza sekta ya kilimo na kutoa ujumbe kwa vijana
kuona umuhimu wa kilimo hasa kilimo cha biashara.
“Sheria
na tamaduni zilizopo zinakwaza juhudi za mwanamke kupata fursa za kiuchumi kwa
sababu hawana haki ya kumiliki ardhi au vifaa vya kilimo, vyanzo endelevu vya
maji, ukosefu wa mikopo ambayo wanahitaji ili kufanikisha juhudi zao”alisema
Kasuga.
Kwa
upande wake mwakilishi kutoka shirika la msaada la Marekani (USAID) Randy
Chester alisema kuwa mchezo wa KUMEKUCHA umeandaliwa na taasisi ya Africa Lead
kwa kushirikiana na Media for Development International (MFDI) na kufadhiliwa
na USAID kwa lengo la kupunguza uhaba wa vyakula vyenye virutubisho hapa
Tanzania.
Mchezo
wa KUMEKUCHA ni mchezo wa redio wa kila wiki ambao unaangazia maisha, vikwazo
na fursa za wakulima Tanzania na utaanza kurushwa hewani kuanzia Julai 25, 2016
kupitia Redio Free Afrika, Redio Abood FM, Redio Ebony FM na Redio Bomba FM.



