Kutoka Simiyu: DED Bariadi Amtumbua Mkuu Wa Shule Kwa Kufanya Mapenzi Na Wanafunzi Wake.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu,
Abdalah Malela amemvua madaraka Mwalimu Mkuu Masunga Ng’waya wa Shule ya Msingi
Mwashagata, iliyopo kijiji hicho kata ya Ihusi kwa kosa la ukosefu wa maadili.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi jana, mkurugenzi huyo alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni la
baada ya mwalimu mmoja wa shule yake kumrubuni mwanafunzi wake kwa kufanya mapenzi naye tena kwenye nyumba yake, kitendo ambacho
ni cha kukosa maadili.
“Imebainika
hili ni tukio la nne kwa mwalimu huyo kutuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi
tofauti tofauti lakini amekuwa hachukuliwi hatua, lakini mimi kwa mujibu wa
sheria nimemvua madaraka mwalimu mkuu huyo ili awe mwalimu wa kawaida, sababu
amekosa maadili ya kuendelea kushika wadhifa huo,” alisema mkurugenzi huyo.
Aidha, alisema kesi hiyo tayari imefikishwa polisi na wakati
wowote mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani. Katika hatua nyingine, Mkuu wa
Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alisikitishwa na kitendo hicho na kumtaka
mkurugenzi wa halmashauri hiyo kumchukulia hatua na kuwashauri wazazi wamuache
mwanafunzi huyo aendelee na masomo yasije yakampita huku hatua za kisheria kwa
mtuhumiwa zikiendelea.
Mlezi wa mwanafunzi huyo, alisema mwanawe alisimama masomo kwa
muda wa wiki mbili kutokana na tukio hilo. Mwalimu Ng’waya alipozungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya
simu alikiri kuvuliwa madaraka na kueleza amekuwa mwalimu wa kawaida huku
akiendelea kufundisha katika shule hiyo.
Chanzo-Habarileo



