Lindi Watakiwa Kushiriki Katika Zoezi La Umezaji Kingatiba kwa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele

WAKAZI wa Lindi na vitongoji vyake wametakiwa
kushiriki katika kampeni ya kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele
kwa kumeza kingatiba za kutokomeza magonjwa hayo pamoja na kutunza mazingira
kwa kuondoa mazalia ya mbu wanaenezao magonjwa hayo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa
kambi ya upasuaji wa Mabusha na Ngirikokoto(Henia) unaofanyika mkoani Lindi.
"Wakazi wa Lindi na Vitongoji vyake
tunatakiwa kushiriki katika zoezi la kumeza dawa za kukinga magonjwa yaliyokuwa
hayapewi kipaumbele pamoja na kufanya usafi wa mazingira ili kuondoa mazalia ya
mbu"alisema Dkt. Ndugulile

Aidha, Dkt. Ndugulile amewataka wananchi wa
Lindi kuondoa dhana potofu ya kuwa kila mwenye mabusha au ngirimaji basi
atakuwa amerogwa ila ajue ugonjwa huo unasababishwa na vimelea vinavyotokana na
mbu na kuzingatia umezaji wa dawa hizo.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika
kuhakikisha wanapambana kutokomeza ugonjwa huo Serikali kwa kushirikiana na
Kampuni ya Utafiti ya uchimbani mafuta na gesi ya Statoil wamepata fedha za
kuwafanyia upasuaji wagonjwa 200 wa mabusha na ngirikokoto kwa awamu ya kwanza
ya mwaka 2017 na wagonjwa 200 kwa awamu ya pili ya mwaka 2018.

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa
wananchi wa Lindi wanatakiwa kutoa taarifa sehemu husika pindi wanapoambiwa
kuwa dawa muhimu hakuna kwenye vituo vya afya vya Serikali kwani dawa hizo zipo
kwa asilimia 90 Mkoani humo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa
Lindi Bw. Ramadhani Kaswa amesema kuwa umezajii wa kingatiba ya magonjwa hayo
umefikia asilimia 70 kwa mwaka 2016/2017.

Aidha, Bw. Kaswa amesema kuwa kutokana na
zoezi la kuwatambua wagonjwa wenye mabusha na ngirikokoto wamejiandikisha
wagonjwa 1294 kwa mkoa wa Lindi ikiwemo Manispaa ya Lindi wagonjwa 67,Wilaya ya
Nachingwea wagonjwa 101,Halmashauri ya Lindi wagonjwa 633, Wilaya ya Liwale
wagonjwa 387 na Wilaya ya Luongo wagonjwa 106.
Uzinduzi huo uliambatana na zoezi la kumeza
Kingatiba za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo mabusha na
matende,usubi,minyoo,trakoma(vikope) na vichocho.



