CUF YA MAALIM SEIF YACHEKELEA MAULID MTULIA KUJIUZULU UBUNGE
Naibu katibu mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui
Uamuzi wa Maulid
Mtulia kujivua ubunge na uanachama haujakishtua chama chake cha CUF, badala
yake kimesema bado wengine wawili ambao kingependa waondoke haraka.
Hilo lilisemwa jana
na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaongoza upande mmojapo
kati ya mbili zinazokinzana. Upande mwingine unaongozwa na Profesa Ibrahim
Lipumba.
Naibu katibu mkuu
wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema kuwa, Mtulia ni mmoja wa wabunge
watatu wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.
“Hatukutarajia kama
Mtulia ataondoka wakati huu, bali tulijua ataendelea kudumu. Lakini kama
ameondoka ni faraja kwetu kwa sababu katika mipango yetu tulishamuondoa,”
alisema Mazrui.
“Tunawaombea dua
wale wawili waliobaki waondoke hata leo kwa sababu kuendelea kukaa kwao ndani
ya CUF ni kukidhoofisha chama hiki.”

Aliyekuwa mbunge wa kinondoni Maulid Mtulia
Mazrui aliwataka
wabunge kutoshangaa endapo wenzao hao watatangaza kujiuzulu nafasi zao akidai
kuna mipango inaendelea kupangwa ili kufanikisha mchakato huo.
“Narudia tena na
waondoke, tena waondoke haraka. Ninawahakikishia wana CUF kuwa chama hiki kipo
imara na wasiwe na hofu,” alisema Mazrui.
Alisema CUF ni
taasisi imara na kati ya wabunge 40, watatu alidai wamekuwa wakikivuruga chama
hicho kwa kushirikiana na Profesa Lipumba.
Akizungumzia
kuondoka kwa Mtulia, alisema wakati mwingine akifa mgonjwa uliyemuuguza muda
mrefu unamshukuru Mungu.
“Tunamshukuru Mungu
maana tumeuguza vya kutosha. Haikuwa bahati yetu,” alisema.




