HATIMA YA WABUNGE WAWILI WA CHADEMA KUJULIKANA LEO.....NI BAADA YA JANA KURUDISHWA RUMANDE

Wabunge Susan Kiwanga na Peter
Lijualikali waliofikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro
pamoja na washtakiwa wengine 36 walirejeshwa rumande.
Mahakama iliyokuwa itoe uamuzi wa
dhamana jana Jumanne Desemba 5,2017 ilikwama kufanya hivyo kutokana na
kuibuka hoja za kisheria.
Upande wa mashtaka na ule wa utetezi
unavutana kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani
hapo.
Kutokana na mvutano wa kisheria,
hakimu Ivan Msack aliahirisha kesi hiyo hadi leo Jumatano Desemba 6,2017 ili
kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka
nane likiwamo la kuchoma moto ofisi ya Kata ya Sofi iliyopo wilayani Malinyi.
Washtakiwa wanatetewa na mawakili Peter
Kibatala, Ignas Punge, Fredrick Kiwelo na Bartholomew Tarimo.
Upande wa mashtaka unawakilishwa na
mawakili wa Serikali, Edga Bantulaki na Sunday Hyera.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Frederick Sumaye walihudhuria
mahakamani.
Wengine waliofika mahakamani ni
mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Viti Maalumu, Devota Minja.



