Mfanyakazi Wa Mfuko wa PPF Adakwa Akisafirisha Mirungi

Polisi mkoani Kilimanjaro
inamshikilia mfanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PPF) kwa tuhuma za
kusafirisha dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis
Issah alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Anitha Oswald (32).
“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald,
ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za
kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370 kwa kutumia gari lake analomiliki
aina ya Toyota Sienta rangi ya silva,” alisema kamanda Issah.
Kamanda Issah alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa
eneo la Majengo kwa Mtei Desemba 19 akitokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo
huo.
“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini,
operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika
kujihusisha na biashara hii”, alisema.
Kamanda huyo alisema polisi wanaendelea
kumtafuta dereva wa gari hilo ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza
lilipogonga mti wakati akiwakimbia askari.



