RC GAMBO AMTOA HOFU RAIS MAGUFULI KUHUSU MAANDAMANO YA MANGE KIMAMBI

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho gambo
amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
kutotishwa na maandamano ya mitandaoni yanayoratibiwa na Mange Kimambi, kwani
mkoa wa Arusha uko salama.
Mrisho Gambo ameyasema hayo leo
alipokuwa akitoa salam zake kwa Rais Magufuli, kwenye sherehe za uzinduzi wa
nyumba za polisi mkoani Arusha, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abedi.
Kwenye salamu hizo Mrisho Gambo
amesema mkoa wa Arusha ni salama na wakazi wa Arusha hawana haja ya maandamano,
kwani wanachohitaji ni uongozi wake ambao unawaletea maendeleo makubwa.
Mrisho gambo aliendelea kwa kueleza
kuwa anatambua kazi ya kubwa aliyonayo Rais ya kupigana vita ya uchumi, na watu
wengi wasiopenda nchi hii watachukia kutokana na hilo.
“Mheshimiwa Rais nikuhakikishie tu
Arusha ni salama, wala usitishwe na mbwembwe za kwenye mitandao, watanzania
halisi ni hawa hapa wenye Arusha yao.
"Watanzania wa Arusha wamechoka
na maandamano, wanataka uongozi wa kwako ambao unawaletea maendeleo. Ninajua
vita uliyokuwa nayo ni kubwa sana, Mwl. Nyerere alikuwa na vita ya ukombozi,
akaimaliza salama,
"Mheshimiwa Rais vita yako wewe
ni ya kiuchumi, ni vita inayopigana na mabeberu ambao wanawatumia wengine
kukwamisha jitihada zako. Watu wengi ambao hawaitakii mema nchi hii hawawezi
kuipenda”, amesema Mrisho Gambo.
Sambamba na hilo Mkuu wa mkoa huyo wa
Arusha amemshukuru Rais Magufuli na wadau kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo
za askari polisi, ambazo awali ziliteketea kwa moto.



