RC Makonda Awajibu Mawaziri Waliompinga.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
amesema wale wote wanaosema kampeni yake ya kuwasaidia akina mama
waliotelekezwa na watoto imevunja sheria, pengine wana watoto nje na wanaogopa
kujitokeza.
Makonda ameyasema hayo leo Aprili 19,
katika uzinduzi wa hospitali ya kisasa ya mama na mtoto iliyopo Chanika
iliyojengwa kwa msaada wa Shirika Maendeleo la Kimataida la Korea (Koica).
“Eti wanasema navunja sheria,
natakiwa nifanye faragha kama unataka faragha tunza mtoto. Mimi siogopi, nipo
tayari kufungwa lakini kwa ajili wa kutetea haki za watoto. Pengine hao
wanaosema navunja sheria wana watoto wao nje wanaogopa kujitokeza,” amesema.
Jana, Waziri wa Sheria na Katiba,
Profesa Palamagamba Kabudi akiwa bungeni alisema kampeni hiyo inaweza
kuleta hali ya sintofahamu na akabainisha kuwa inapaswa kufanyika faragha na
sio kama inavyofanyika sasa.
Awali, Waziri wa Afya, Jinsia,
Wanawake na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kampeni hiyo ni sahihi ila
kasoro yake ni kutokuwa na faragha, lakini akasema kwa sasa inafanyika huku
picha za watoto zikifichwa.
Aliyeibua hilo bungeni jana alikuwa
ni mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliyehoji uhalali wa kampeni hiyo na
akahoji kama haivunji sheria na kuwavunjia haki wanawake na watoto.



