Kambi Ya Upinzani Waitaka Serikali Kuwasikiliza Marais Wastaafu JK Na Mkapa

Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, wameitaka Serikali kutilia mkazo ushauri uliotolewa na marais
wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wa kuwapo kwa mjadala wa kitaifa wa
elimu.
Wakizungumza leo
Mei 5, 2018 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, wabunge wa upinzani wamesema
hali ya elimu ni mbaya na Serikali inaandaa kizazi kijacho kisichoweza
kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Mbunge wa Vunjo
(NCCR-Mageuzi), James Mbatia amesema, “Taifa lolote lile ambalo halijui umuhimu
au halipendi kuwekeza katika elimu ni Taifa mfu, ukitaka kuua elimu yetu basi
usiwekeze katika elimu.”
Mbatia ambaye ni
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa amesema, Taifa hili limebahatika kuwa na marais
walimu isipokuwa Mzee Mkapa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni Mwalimu, ‘First
Lady’ Janeth Magufuli ni mwalimu.
“Leo Tanzania tupo
wapi? Na rasilimali kubwa kuliko zote duniani ni rasilimali watu na rasilimali
watu tuliyonayo sasa haijitambui na ili ilijitambue lazima iwe na ufahamu.
“Kama Rais Mkapa
anaomba mjadala wa elimu na amekuwa akilirudia mara kwa mara. Rais Kikwete
amezungumza haya. Rais Mwinyi amesema nchi inaongozwa kama gari bovu. Mwalimu
Nyerere alilisema hadi anaingia kaburini,” amesema Mbatia na kuongeza:
“Tuwe na mjadala
mpana wa kitaifa, Tanzania ni yetu sote, watoto hawa wanaumia, hivi ukweli
watoto wa rais wetu wanasoma katika shule hizi hizi, hebu tumwogope Mwenyezi
Mungu.”
Mbatia amesema
vitabu vinavyosambazwa sasa shule za msingi ni vibovu na kumtaka Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako kuacha kutoa vitisho kwa
watu kuwa watachukuliwa hatua na badala yake, “ajiulize tatizo lipo wapi, nani
kalisababisha.”
Naye Waziri kivuli
wa elimu, sayansi na teknolojia, Susan Lyimo amesema; “Hakuna nchi yoyote
iliyoendelea pasina kuwekeza katika elimu, lakini kinachofanyika sasa, ingawa
Serikali haitaki kusikia ila hali ya elimu ni mbaya.”



