Mbwa Wazua Mvutano Katika Kikao Cha Madiwani
Uamuzi wa
wataalamu wa mifugo kuwaua kwa kuwapiga risasi mbwa wote wanaozurura mitaani
umepingwa katika Wilaya ya Siha na kusababisha baadhi ya viongozi wa kisiasa
kutaka zoezi hilo lisitishwe na wanyama hao kupatiwa chanjo.
Katika Kikao cha
Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, baada ya Diwani wa Kata ya Karansi
(CCM), Dancan Urassa aliitaka idara ya mifugo kuwaua kwa risasi mbwa wote
wanaozurura mitaani kwa kukosa uangalizi, ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa
kichaa cha mbwa unaosababishwa na virusi vinavyoshambulia mfumo wa fahamu na
ubongo.
Hata hivyo hoja
hiyo, ilipingwa vikali na Diwani wa Kata ya Kirua (CHADEMA), Robert Mrisho,
aliyedai kwamba hatua hiyo ni kwenda kinyume na haki za wanyama na ni ukatili
dhidi ya wanyama.
“Mimi sikubaliani
na hoja ya kuua mbwa kwa kuwapiga risasi, nadhani njia nzuri na inayokubalika
ni kuwakamata na kuwapa chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa na ndio njia bora ya
kwanza ya kulinda ustawi wa wanyama" amesema .
Ameongeza
"Kama kuna zoezi hilo lisitishwe haraka na wapewe chanjo, ili kuepuka
ukatili dhidi ya wanyama kwa sababu wanayo haki ya kuishi,” alisema Mrisho.
Baada ya mvutano
huo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Frank Kisinani ameunga mkono hoja ya
Diwani wa Karansi na yeye akitaka uamuzi wa kuwapiga risasi ubaki kama ulivyo
hata kama haki za wanyama zinakataza kuua wanyama.



