Waziri Mkuu Majaliwa atoa siku tatu kwa wafanyabiashara kusambaza mafuta ya kula nchini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa
siku tatu kwa kampuni za mafuta ya kula nchini kuingiza bidhaa hiyo sokoni na
kuonya kuwa baada ya muda huo kupita, Serikali itapita viwandani na katika
bohari za mafuta kufanya tathmini.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo jioni
Mei 9, 2018 bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu agizo la Spika wa Bunge, Job
Ndugai ambaye jana aliitaka Serikali kutoa majibu kuhusu madai ya kupanda kwa
bei ya mafuta baada ya baadhi ya wabunge kuhoji jambo hilo na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kutoa majibu ambayo
hayakumridhisha.
“Serikali tunatoa siku tatu kuanzia
kesho kwa mafuta yote yaliyoko katika bohari kuu ambayo tunajua yapo ili
Watanzania wasihangaike kununua kwa bei ya juu, mafuta yaliyoko bandarini
yanaendelea na taratibu zake,”amesema Majaliwa.
Amesema Serikali itaendelea
kuzungumza na wafanyabiashara walio na mafuta bandarini kuondoa mafuta yao ili
yaweze kusambaa sokoni ili watu wapate mafuta.
“Kuanzia Jumapili tutalazimika
kuingia viwandani na kuhakiki kama mafuta yapo ama hayapo,”amesema.
Awali, Mwijage amesema mahitaji ya
mafuta nchini ni kati ya tani 400,000 hadi 450,000 na kwamba vyanzo vya mafuta
nchini vinatosheleza asilimia 30 ya mahitaji huku asilimia 70 ikiagizwa kutoka
nje ya nchi.
Amesema mafuta yanayoagizwa kutoka
nje ya nchi ni yaliyosafishwa na yale ambayo hayajasafishwa.
Amesema mwaka jana kampuni binafsi
ambazo ndizo zinazoingiza mafuta kwa ajili ya kusafisha katika viwanda
vilivyoko nchini, yaliingiza tani 344,369.5 ikiwa ni wastani wa tani 28,697 kwa
mwezi.
Amesema Januari hadi Machi, 2018
kiasi kilichoagizwa cha mafuta kutoka nje ya nchi ni tani 30,210.71 na kwamba
kwenye hifadhi kuna tani 68, 902 za mafuta.



