Baada Ya Wapinzani Kuitwa Mbwa. Spika Ndugai Aibuka Ghafla Na kumpokonya Mwenyekiti Uongozi,

Spika Job Ndugai leo amelazimika
kumpokonya Najma Giga uongozi wa kikao cha Bunge baada ya mzozo uliosababishwa
na mbunge wa CCM aliyewafananisha wapinzani na mbwa.
Spika Ndugai alifanya kitendo hicho
kisicho cha kawaida katika kikao cha 44 cha Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge
wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya mwaka 2018/19 ya Wizara ya Fedha na
Mipango.
Wakati akichangia, mbunge huyo wa
Jang’ombe, Ali Omar alisema: “Ukiona majuha wanapongezana wakaona wamefanya la
maana, kuna hawa mbwa kama tutawatoa itakuwa vizuri sana. Nasikia milio ya mbwa
ukiwatoa itakuwa vizuri.”
Baada ya kauli hiyo, wabunge wawili
kutoka Chadema, Joseph Selasini (Rombo) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa
Mjini) walisimama kutaka utaratibu ufuatwe kwa mchangiaji kuomba radhi.
Hata hivyo, Giga hakuruhusu hilo na
kusababisha wabunge wengine wa upinzani kupiga kelele wakimtaka mbunge huyo
afute kauli hiyo.
Giga alitumia kama dakika mbili
kuwazuia lakini hakuweza na kumtaka Omar aendelee kuchangia.
Hata hivyo hakuweza kuwazuia kutokana
na wabunge hao wa upinzani kuendelea kupiga kelele wakisisitiza Omar
ashinikizwe kufuta kauli yake.
Wakati kelele zikiendelea na utulivu
bungeni ukitoweka, Spika Ndugai akaingia na kuchukua uongozi wa kikao na hivyo
Giga, aliyeanza kuongoza kikao hicho tangu asubuhi, kulazimika kumuachia
uongozi.
Credit: Mwananchi



