WANANCHI ZAIDI YA 400 WAJITOKEZA KUUNGANISHWA MAJISAFI BANGULO
Wakazi zaidi ya 400 wa Mtaa wa Bangulo, Kata ya Pugu Stesheni wamejitokeza kuomba huduma ya majisafi baada ya kukamilika kwa Mradi wa Usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini maarufu kama Bangulo uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA)
Afisa Huduma kwa Wateja DAWASA Mkoa wa kihuduka DWASA Ukonga, Ndugu Valence Lyamuya amesema kuwa tangu kuanza kwa majaribio usambazaji maji katika maeneo yaliyopitiwa na mradi, mwitikio mkubwa wa Wananchi zaidi ya 400 wamejitokeza kuomba kuunganishwa na huduma ya maji.
"Kwa kipindi kirefu sana wananchi wa Mtaa wa Bangulo wamekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji na Serikali kupitia Wizara ya Maji chini ya Usimamizi wa DAWASA ilikuja na utekelezaji wa Mradi huu wa Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) na wananchi wamehamasika kuomba kuunganishiwa huduma. Hadi sasa tumepokea maombi ya wateja wapya zaidi ya 400 kutoka katika Mtaa wa Bangulo na Wateja …wameshaunganishwa huduma" Amesema Lyamuya.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Bangulo ndugu Goodluck Mwele amesema Mradi wa Maji Bangulo unaenda kuboresha maisha ya wananchi kwa kuondoa tatizo la wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji na kupunguza gharama za maisha kupitia upatikanaji wa majisafi na salama katika Mtaa huo.
"Tunaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo kupitia DAWASA wametuletea mradi huu ambao umekuwa mkombozi kwa wananchi, awali wananchi wamekuwa wakipata huduma ya maji kupitia Visima binafsi waliokuwa wakiwauzia kwa bei ghali na vilivyo mbali, na wengine wakinunua maji kwa gharama ya Shilingi 15,000 kwa uniti moja na baada ya huu mradi DAWASA wanawauzia maji yao kwa Shilingi 1,679 kwa unit moja hivyo kuokoa muda na pesa nyingi." amesema Mwele.
Kwa upande wake Mkazi wa Mtaa wa Bangulo kwa Msafiri Bi. Zubeda Saidi ameshukuru uwepo wa Mradi huo wa maji na kwani kwa muda mrefu walikuwa wanateseka na adha ya ukosefu wa majisafi na salama.
"Kwa sasa tunashukuru maji yapo yanapatikana vizuri na kwa muda wote bila ya wasiwasi, wananchi tumefurahi na tunaomba DAWASA iongeze kasi katika kutuunganishia huduma kwa kuwa watu wengi bado wanasubiri kupata huduma hii muhimu. Amesema Zubeda.
DAWASA inaendelea na zoezi la maunganisho mapya ya huduma kwa wateja wapya sambamba na kutoa elimu juu ya huduma za Maji ikiwemo matumizi sahihi ya huduma, taarifa za maunganisho mapya na taarifa nyingine muhimu




