PROF MKENDA: SERIKALI KUBORESHA MIFUMO YA TAKWIMU YA SEKTA YA ELIMU
Dar es salaam - Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali inatarajia kuanzisha mfumo shirikishi wa tafiti za elimu ili kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, na usimamizi wa takwimu ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wadau wa elimu nchini
Akizungumza wakati akifungua kongamano kati ya Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu (HELSB) na Taasisi ya Adapt IT (Adapt IT and HESL Technology Symposium), amesema lengo kuu ni kuwezesha matokeo ya tafiti zinazofanyika kuwa na tija.
"Serikali tayari imeunda kamati ya wataalamu yenye jukumu la kupitia mifumo iliyopo na kuandaa mapendekezo ya uboreshaji, kwa lengo la kukamilisha mapendekezo ya ujenzi wa mfumo wa takwimu wa sekta ya elimu". Alisema Profesa Mkenda
Alisema mfumo huo utakapo kamilika utawezesha upatikanaji wa takwimu zote za sekta ya elimu pia mfumo huo utakuwa na uwezo wa kupokea takwimu mbalimbali zinazohusiana na elimu kutoka katika mifumo mingine ya Serikali ikiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Awali akizungumza katika ufunguzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Dokta Bill Kiwia, amesema kupitia Kongamano hilo wataangalia namna ADAPT IT ambao tayali wana uzoefu na teknolojia ya kutosha wamekumbana na changamoto zipi kwa lengo la kuja na mifumo bora hili kusaidia upatikanaji wa huduma bora hususani kwa wanafunz kwa lengo la kupunguza gharama kwa Serikali.
“Tumekuwa tukijenga mifumo yetu ya ndani kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani maana hili ndilo lengo la serikali la kutaka mifumo isomane. Katika sekta ya elimu pia mifumo yetu inaenda kusomana kutokana na hatua zinazochukuliwa,”. Alisema Dkt. Kiwia










