Breaking News

TAHLISO YAPONGEZA SERIKALI KWA KUONGEZA IDADI YA WANUFAIKA WA MIKOPO ELIMU YA JUU

Dar es salaam - Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua yake ya kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza mapema leo Mei 15, 2025 na Rais wa TAHLSO, Geofrey Kiliba amesema uamuzi huo ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuwekeza kikamilifu katika elimu ya juu na kusaidia vijana wengi zaidi kutoka familia zenye kipato cha chini kupata elimu.

Kilibi ameeleza kuwa katika bajeti hiyo idadi ya wanafunzi wa mikopo ya elimu ya juu inatarajia kuongezeka kutoka 245,314 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 hadi wanafunzi 252,773 kwa mwaka wa fedha ujao wa 2025/2026.

"TAHLISO tunaipongeza Serikali kwa kusikiliza sauti ya wanafunzi na kuongeza bajeti ya mikopo. Hili ni jambo muhimu sana linaloonesha kuwa Serikali inatambua nafasi ya elimu katika maendeleo ya taifa letu," amesema Rais Kiliba.

Katika hatua nyingine Kiliba, amewakosoa vikali baadhi ya Watanzania wanaoikosoa na kuidharau elimu ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa lina kila sababu ya kujivunia maendeleo yaliyopatikana katika sekta hiyo, hasa chini ya serikali ya awamu ya sita.

Amepongeza serikali kwa hatua thabiti ilizochukua kuboresha elimu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu, kuongeza bajeti ya elimu, na kuwekeza katika maendeleo ya walimu na wanafunzi.

Kiliba pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na wadau wengine wa elimu katika kuhakikisha ubora na usawa wa elimu kwa Watanzania wote.

Amebainisha Kuwa, Nchi ya Tanzania ni kinara kwa Nchi za Afrika Mashariki katika kujali na Kulinda Maslahi ya Elimu hususan ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Akitoa mfano wa Nchi ya Rwanda, Kiliba amesema Kuwa, Nchi hiyo imetoa mikopo 40% Kwa wanafunzi wote waliohitaji ambapo ni kiwango kidogo kulinganisha na hapa nchini.

" Elimu ya Tanzania imeboreshwa sana alafu Kuna mtu anasimama Jukwaani na Kusema Elimu ya Tanzania ni Matope, Hilo ni pepo likemee".Alisema Kiliba.