Breaking News

ERIC SHIGONGO AZINDUA MADARASA YA KIDIJITALI BUCHOSA – MAPINDUZI YA ELIMU VIJIJINI YACHANUA

Buchosa, Tanzania – Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, wanafunzi wa maeneo ya vijijini sasa wanapata elimu ya sayansi mubashara kutoka kwa walimu walioko jijini Dar es Salaam kupitia teknolojia ya kisasa. Hili limewezekana kupitia Mradi wa Darasa Janja, ubunifu wa kipekee ulioanzishwa na Mbunge wa Buchosa, Mheshimiwa Eric Shigongo.

Mradi huu umebuniwa kwa lengo la kutatua changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika maeneo ya pembezoni, bila kusubiri misaada kutoka kwa wahisani au utekelezaji wa ahadi za kisiasa. Kwa kutumia vifaa vya kisasa kama kamera, projektia, kompyuta na mifumo ya mawasiliano, wanafunzi wa shule mbili tofauti sasa huunganishwa moja kwa moja na walimu walioko mijini, wakijifunza kwa wakati mmoja kana kwamba wote wako katika darasa moja.
Mradi wa Darasa Janja umeleta mabadiliko makubwa kwa walimu na wanafunzi. Walimu wamepata hamasa mpya ya kufundisha, huku wanafunzi wakionyesha ari mpya ya kujifunza. Ndoto zao za kuwa madaktari, wahandisi, wataalamu wa TEHAMA na fani nyingine za kisayansi sasa zinaonekana kufikiwa kwa vitendo.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo, Mheshimiwa Eric Shigongo alisema, “Maendeleo hayawezi kusubiri. Niliona ni wakati wa kuchukua hatua. Kama hatutawekeza kwenye elimu, hatuwezi kuibadilisha jamii yetu. Kupitia Darasa Janja, tunavunja mipaka ya kijiografia na kupeleka elimu bora kila kona ya Buchosa.”
Jamii ya Buchosa imeshuhudia kwa macho yao mabadiliko haya makubwa na ya kihistoria. Mradi huu umethibitisha kuwa mtu mmoja mwenye maono, moyo wa kizalendo, na uamuzi thabiti anaweza kuleta mageuzi ya kweli katika jamii.