KANDA WA CCM, MASELE MASUNGA, ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA SEGEREA
Dar es Salaam — Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanda wa CCM Masele Masunga, amechukua fomu ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Segerea kupitia tiketi ya chama hicho.
Masunga amekabidhiwa fomu hiyo Juni 30, 2025, na Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Sylvester Yared, katika ofisi za chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Masunga amesema kuwa uamuzi wake wa kugombea umetokana na msukumo kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Segerea waliomshauri kuchukua hatua hiyo, wakieleza kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji msukumo zaidi ili kufanikisha maendeleo ya kweli kwa wananchi.
"Maeneo mengi bado yanahitaji nguvu mpya na msukumo wa maendeleo. Wananchi wameonyesha imani yao na kuniomba nigombee ili kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo katika Jimbo letu," alisema Masunga.
Ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Segerea kuwa ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana na hali duni ya miundombinu ya barabara, ambazo anasema anapenda kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka husika endapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi kama Mbunge.
Masunga ameahidi kuwa atakuwa mstari wa mbele kushughulikia kero za wananchi na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.





