PROF. LIPUMBA: BAJETI 2025/26 IMEGEUZWA KAMPENI YA CCM, ATILIA SHAKA PIA TATHIMINI YA MPANGO WA MAENDELEO
Dar es Salaam - Chama cha Wananchi (CUF) kimetoa uchambuzi wa kina wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26, kikieleza kuwa hotuba ya bajeti iliyowasilishwa bungeni imekosa mwelekeo wa maendeleo ya taifa na badala yake kugeuzwa jukwaa la kisiasa kwa ajili ya kampeni za uchaguzi wa mwaka 2025.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo na Idara ya Sera na Uchambuzi wa CUF, chama hicho kimeeleza kuwa bajeti hiyo ni ya mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26), na hivyo ilipaswa kuwa ya kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto zilizojitokeza. Hata hivyo, CUF inadai kuwa tathmini hiyo haikufanyika, badala yake hotuba ilitumika kumpigia debe mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Bajeti hii ni ushahidi wa wazi kwamba serikali imeshindwa kutekeleza Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Taifa, huku sekta muhimu kama viwanda, kilimo, na ajira zikiwa zimedidimia,” ilieleza taarifa hiyo.
Viwanda na Uchumi Vilivyozorota
CUF imesema azma ya Tanzania ya kuwa nchi ya viwanda imeporomoka baada ya mchango wa sekta hiyo kushuka hadi asilimia 7.3 ya Pato la Taifa mwaka 2024, tofauti na lengo la kufikia asilimia 23 ifikapo mwaka 2025. Miradi mikubwa ya kimkakati kama ule wa Liganga na Mchuchuma haijatekelezwa hadi sasa.
Wastani wa ukuaji wa uchumi kwa miaka minne ya Mpango wa Tatu ni asilimia 5.1 tu, tofauti na lengo la asilimia 10, hali ambayo CUF inaitafsiri kama matokeo ya matumizi yasiyo na tija, vitendo vya rushwa, na miradi ya maendeleo inayojengwa lakini haileti matokeo kwa wananchi.
Gharama za Maisha, Ajira, na Riba za Juu
CUF imeeleza kuwa hali ya maisha kwa wananchi wa kawaida imeendelea kuwa ngumu, licha ya serikali kudai kuwa mfumko wa bei uko chini ya asilimia 4. Taarifa hiyo inasema zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hawana ajira zenye kipato cha uhakika, huku wajasiriamali wakikabiliwa na riba za mikopo zinazofikia hadi asilimia 22 kwa mwaka.
“Ni wazi kuwa mazingira ya biashara si rafiki. Watu wanaacha kuwekeza kwa sababu ya ukosefu wa uhakika wa sera, kodi nyingi zisizoeleweka, na riba za benki zinazokatisha tamaa,” imeeleza CUF.
Fedha Zenye Mashaka na Deni la Taifa
Chama hicho pia kimetilia shaka uwezo wa serikali kugharamia miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani, huku zaidi ya asilimia 50 ya mapato yote yakielekezwa kulipia deni la taifa. Kwa mujibu wa CUF, deni limeendelea kuongezeka kwa kasi bila kuwa na uwazi wa matumizi ya mikopo hiyo.
Bajeti ya Kilimo na Elimu Yadidimia
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa sekta ya kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Watanzania walio wengi, imetengewa asilimia 3.2 tu ya bajeti yote – kiwango kilicho chini ya makubaliano ya Maputo ya kutenga angalau asilimia 10. Elimu na afya pia hazijafikia viwango vya kimataifa vya bajeti vinavyopendekezwa.
CUF: Tutatoa Majibu Kupitia Ilani Yetu
Katika hitimisho lake, CUF imetangaza kuwa itatoa Ilani ya Uchaguzi yenye lengo la kuinua ukusanyaji wa mapato ya kodi kufikia asilimia 20 ya GDP na kukuza uchumi kwa asilimia 10 kwa mwaka katika kipindi cha 2026–2030.
“Tanzania haiwezi kuendelea kwa hotuba za sifa na maneno matupu. Tunahitaji bajeti inayogusa maisha ya watu, si bajeti ya kampeni,” imesisitiza CUF.




