ACT WAZALENDO YAKAMILISHA SIKU 15 ZA OPERESHENI MAJIMAJI, WATAJA CHANGAMOTO SITA WALIZOKUTANA NAZO
Dar es Salaam – Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Operesheni Majimaji, kampeni ya siku 15 iliyolenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kulinda kura kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza na wanahabari leo, Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho, Ndugu Isihaka Mchinjita, amesema operesheni hiyo ilianza rasmi tarehe 1 Julai 2025 na kuhusisha mikutano ya hadhara, vikao na mikutano ya ndani katika mikoa 15 ya Tanzania Bara, ikiwemo Kigoma, Arusha, Ruvuma, Tanga, Mtwara, Tabora na mikoa mingine.
Kwa mujibu wa Mchinjita, Operesheni Majimaji iliongozwa na viongozi waandamizi wa chama akiwemo Kiongozi wa Chama Bi. Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti Bara, pamoja na Kiongozi Mstaafu Ndugu Zitto Kabwe. Lengo kuu lilikuwa ni kuhamasisha wananchi kulinda kura zao na kutoa sauti ya upinzani dhidi ya kile walichokiita udhalimu wa serikali ya CCM.
Katika taarifa hiyo, ACT Wazalendo wamesema hali ya nchi kwa sasa ni ya huzuni, wakibainisha changamoto sita kuu zilizojitokeza wakati wa operesheni hiyo:
1. Umasikini na hali duni: Chama hicho kimeeleza kuwa umasikini umekithiri nchini, huku wakidai idadi ya Watanzania maskini imeongezeka kutoka milioni 12 hadi milioni 26 kati ya 2020 hadi 2025. Wamesema hali hiyo ni matokeo ya sera dhaifu za serikali ya CCM.
2. Ukatili katika sekta ya afya: ACT Wazalendo wameeleza kuwa huduma za afya hazitekelezi tena ahadi ya huduma bure kwa watoto, wazee na wajawazito. Wamedai kuwa huduma hizo zimekuwa chanzo cha manyanyaso na rushwa kwa wananchi maskini.
3. Elimu isiyofungua maisha: Wamesema mfumo wa elimu umeporomoka na watoto wanalazimika kubeba mahindi, maji na kulipia michango licha ya kauli ya “elimu bure.” Walibainisha uhaba mkubwa wa madawati, walimu, madarasa na vyoo katika maeneo mbalimbali waliotembelea.
4. Kilimo kisicho na tija: Chama hicho kililalamikia kushuka kwa bei ya mazao kama pamba na korosho, ucheleweshaji wa malipo, na udhibiti wa serikali usio na tija katika sekta ya kilimo. Walisema wakulima wa chai wa Tanzania hupata asilimia 10 tu ya bei ya soko la dunia ikilinganishwa na asilimia 60 kwa wenzao wa Kenya.
5. Migogoro ya ardhi: ACT Wazalendo wamesema kuwa serikali ya CCM imeongeza maeneo ya hifadhi hadi kufikia asilimia 50 ya ardhi yote ya nchi, hali inayochochea migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Wamedai wananchi wanapokonywa ardhi yao na kuishi kama wakimbizi kwenye ardhi yao wenyewe.
6. Mauaji, vitisho na ukandamizaji: Wamesema matukio ya mauaji na ukatili dhidi ya raia yameshuhudiwa wakati wa ziara yao, huku polisi wakituhumiwa kuwaandama viongozi na wanachama wa chama hicho. Wameeleza kuwa vitendo hivyo havikubaliki na vinaonesha ukosefu wa demokrasia.
ACT Wazalendo wameeleza kuwa ziara hiyo imewapa msukumo zaidi wa kushiriki uchaguzi wa 2025 kwa nguvu mpya, wakiahidi kuongoza mapambano ya kisiasa kwa ajili ya taifa huru, lenye haki, usawa na maendeleo kwa wote. Wamesisitiza kuwa moto wa Operesheni Majimaji hautazimika hadi pale madai ya wananchi yatakapotimizwa.
“Tumechoka kuishi kama mateka katika nchi yetu. Operesheni Majimaji imetufungua macho na kutupa kila sababu ya kuingia kwenye uchaguzi kimapambano. Tutaendelea kulinda kura hadi ushindi utapatikana,” alisema Mchinjita.
Chama hicho kimewataka Watanzania kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa mwaka 2025, huku wakihimiza umoja, mshikamano na ushirikiano kati ya makundi yote ya kijamii.




