Breaking News

DCEA YAELIMISHA UMMA KUHUSU DAWA ZA KULEVYA MAONYESHO YA SABA SABA

Dar es salaam - Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inashiriki katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya na sheria zinazozihusu.

Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuwa ushiriki huo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuelimisha jamii kuhusu aina za dawa za kulevya, athari zake, na hatua za kisheria dhidi ya wanaojihusisha nazo.

“Tupo hapa kuwapa wananchi elimu ya kutosha kuhusu dawa za kulevya, madhara yake, na kufahamu sheria zinazodhibiti matumizi, usambazaji, na umiliki wa dawa hizo,” amesema Kamishna Lyimo.
Ameongeza kuwa DCEA inaendesha oparesheni maalum katika shule na vyuo kwa lengo la kutoa elimu ya kinga kwa vijana, sambamba na oparesheni za kuwasaka wafanyabiashara wa dawa hizo haramu nchini kote.

Aidha, Kamishna Lyimo amesema serikali ya awamu ya sita inatoa huduma za matibabu bure kwa waathirika wa dawa za kulevya ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida na kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Amebainisha kuwa jitihada hizo zimefanikisha kupungua kwa upatikanaji wa dawa hatari kama heroin na cocaine, na kuwataka wananchi kutembelea banda la DCEA katika maonesho hayo kwa elimu zaidi.

Maonesho hayo yataendelea hadi Julai 13.