INEC YAKUTANA NA WAWAKILISHI WA VIJANA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU 2025
Dar es salaam - Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mheshimiwa Balozi Omar Ramadhan Mapuri, leo Julai 31, 2025, amefunga rasmi Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliwakutanisha Tume na wawakilishi wa vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujadili masuala muhimu yahusuyo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akihutubia wakati wa kufunga mkutano huo, Mhe. Balozi Mapuri aliwataka vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kuhamasisha amani, mshikamano na uzalendo. Alisisitiza kuwa sauti ya vijana ni muhimu katika kuimarisha demokrasia na kwamba Tume itaendelea kushirikiana nao katika hatua mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu.
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Tume kuhakikisha kuwa makundi yote ya kijamii, hususan vijana, yanashirikishwa kikamilifu katika masuala ya uchaguzi ili kujenga misingi imara ya ushiriki wa wananchi katika uongozi wa taifa.







