Breaking News

MAHAKAMA YAZIMA MPANGO WA ACT - WAZALENDO KUPORA OFISI YA CUF KILWA

Lindi - Chama Cha Wananchi (CUF) kimeibuka na ushindi katika kesi ya madai iliyofunguliwa na chama cha ACT-Wazalendo kuhusiana na umiliki wa Ofisi ya CUF iliyoko Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa taatifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Julai 30, 2025 na kitengo cha habari cha chama hivho imesema kesi hiyo (Madai Na. 10 ya 2024), ACT-Wazalendo walidai kuwa ofisi hiyo ni mali yao, wakieleza kuwa walipewa na aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Mheshimiwa Seleman Bungara (maarufu kama Bwege). Hata hivyo, Mahakama imetupilia mbali madai hayo na kuthibitisha kuwa ofisi husika ni mali halali ya CUF – Chama Cha Wananchi, baada ya kujiridhisha kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa utetezi.

Tukio hili linatokana na mvutano uliotokea mapema mwaka 2024, ambapo ACT-Wazalendo walivamia eneo la ofisi ya CUF na kuanzisha ujenzi bila ridhaa ya wamiliki halali. Aidha, walipanga kufanya uzinduzi wa ujenzi huo kinyume cha sheria, tukio ambalo lilitarajiwa kuongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman.

Hata hivyo, mpango huo ulizimwa na CUF, hatua iliyosababisha upande wa ACT-Wazalendo kufungua kesi mahakamani. Kwa uamuzi huu wa Mahakama, ni dhahiri kuwa juhudi za ACT-Wazalendo kujimilikisha ofisi hiyo zimegonga mwamba na haki imetendeka kwa mujibu wa sheria.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Chama Cha Wananchi kinapenda kuwashukuru wanachama wake na wananchi wote kwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuamini katika mfumo wa haki na utawala wa sheria.