Breaking News

RAIS MWINYI: HAYATI MZEE MKAPA NI MFANO WA KUIGWA KWA MCHANGO WAKE

Masasi, Mtwara – Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Hayati Benjamin William Mkapa atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha misingi ya maendeleo, utawala bora na ustawi wa Taifa la Tanzania.

Akizungumza katika Ibada Maalum ya Kumbukumbu ya Miaka Mitano ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika leo katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, Dkt. Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu ilijenga nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani, na mshikamano miongoni mwa Watanzania, pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika bara la Afrika na ulimwenguni. Alimwelezea Hayati Mkapa kama kiongozi aliyekuwa na dira, msimamo na uzalendo wa kweli.

Aidha, Dkt. Mwinyi alikumbusha kuwa Hayati Mzee Mkapa alikuwa muumini wa ujamaa na uchumi wa soko unaoongozwa na sekta binafsi, huku akihakikisha kuwa maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi. Alibainisha kuwa Mkapa ndiye aliyeanzisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, ambayo imekuwa mwongozo muhimu wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii, na imewezesha uzinduzi wa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Katika hotuba yake, Rais Mwinyi alitoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wanahabari kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuendeleza tunu ya amani kama njia bora ya kumuenzi Hayati Mkapa. Alisema Watanzania wanayo sababu ya kujivunia viongozi waliopo kwa kuendeleza misingi na maono ya waasisi wa Taifa.

Mara baada ya ibada hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alizuru kaburi la Hayati Mkapa na kuweka shada la maua kwa heshima ya kiongozi huyo mashuhuri, akiwa ameongozana na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mheshimiwa Filipe Nyusi, pamoja na mkewe na mjane wa Hayati Mkapa, Mama Anna Mkapa.
Hayati Benjamin William Mkapa alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020, akiwa na umri wa miaka 81, jijini Dar es Salaam. Ataendelea kukumbukwa kama mmoja wa marais waliotoa mchango mkubwa katika kulijenga Taifa la Tanzania katika misingi ya haki, usawa na maendeleo endelevu.