RAIS SAMIA AAHIDI BILLIONI 1 KWA TAIFA STARS IWAPO WATATWAA UBINGWA WA CHAN 2024
Dar es Salaam — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi donge nono la Shilingi Bilioni 1 taslimu endapo timu ya Taifa, Taifa Stars, itafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya CHAN 2024. Mashindano hayo yatafanyika mwaka huu kwa ushirikiano wa nchi tatu — Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi, amesema ahadi hiyo ya Rais Samia inalenga kuchochea ari na hamasa kwa wachezaji wa Taifa Stars.
"Katika kuchagiza hamasa kwa timu yetu ya Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa ahadi ya Shilingi Bilioni 1 kwa vijana wetu wa Taifa Stars iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa CHAN 2024," amesema Waziri Kabudi.
Ameeleza kuwa Tanzania haikupata nafasi ya kuandaa mashindano haya kwa bahati tu, bali ni matokeo ya uwekezaji mkubwa na juhudi za Rais Samia katika kukuza sekta ya michezo nchini.
Waziri Kabudi pia amesema kuwa maandalizi muhimu kwa ajili ya mashindano hayo yamekamilika, ikiwemo maandalizi ya mchezo wa ufunguzi, malipo ya ada mbalimbali, maandalizi ya viwanja vya michezo na vya mazoezi.
Aidha, Waziri amewahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara na kiuchumi zitakazojitokeza kipindi hiki, hususan katika maeneo ya vyakula, malazi na usafirishaji.
Kwa upande wa hamasa, amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu ya Taifa, kwa kuzingatia kaulimbiu ya mashindano haya: "LINAKUJA NYUMBANI."
Katika kuendeleza burudani na tamaduni, Waziri ametangaza kuwa kutakuwa na CHAN Singeli Festival, tamasha la muziki wa Singeli litakalofanyika siku mbili kabla ya kuanza kwa mashindano, likiwa na lengo la kuutangaza muziki huo kimataifa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa, ametangaza zawadi nyingine ya "Goli la Mama", ambapo Taifa Stars watapokea Shilingi Milioni 10 kwa kila goli watakalofunga katika hatua ya makundi na mtoano. Kiwango hicho kitaongezeka hadi Shilingi Milioni 20 kwa kila goli litakalofungwa kwenye mechi za nusu fainali na fainali.
Mashindano ya CHAN 2024 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 2 Agosti kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam. Timu ya Taifa, Taifa Stars, itafungua dimba kwa kumenyana na Burkina Faso, huku mgeni rasmi wa siku hiyo akiwa ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.





