Breaking News

RAIS WA SHIRIKISHO LA FILAMU TANZANIA, ASHIRIKI MKUTANO WA VIONGOZI WA FILAMU AFRIKA

Kampala, Uganda - Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Bw. Rajabu Amiry, ameshiriki katika mkutano muhimu wa viongozi wa mashirikisho na vyama vya watayarishaji wa filamu (filmmakers) kutoka nchi nane za Afrika uliofanyika jijini Kampala, Uganda.

Katika mkutano huo wa siku tatu, viongozi hao walijadili kwa kina njia za kukuza na kuimarisha sekta ya filamu barani Afrika, huku wakilenga kuongeza ushirikiano baina ya nchi wanachama na kufungua masoko mapya ya filamu kupitia mpango mpya ujulikanao kama Stream East.
Mkutano huo umekamilika kwa mafanikio ambapo mkataba wa makubaliano (MoU) umesainiwa, ukiweka msingi wa ushirikiano rasmi katika kuendeleza na kusambaza kazi za filamu ndani na nje ya bara la Afrika. Hatua hii inalenga kutoa fursa zaidi kwa wasanii, watayarishaji, na wadau wa tasnia ya filamu kupata masoko mapya na jukwaa la kimataifa kwa ajili ya kazi zao.

Bw. Rajabu Amiry ameeleza kuwa makubaliano hayo ni hatua kubwa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kuinua tasnia ya filamu na kuwapa vijana nafasi za ajira kupitia ubunifu wao.