RC CHALAMILA ASIKITISHWA NA HUDUMA MBOVU YA MABASI YAENDAYO HARAKA – DART
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amefanya ziara katika Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka kilichopo Kimara Mwisho, Wilaya ya Ubungo, ambapo ameonesha kutoridhishwa na huduma za usafiri zinazotolewa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kupitia UDART.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, RC Chalamila amesema huduma hiyo imekuwa duni kutokana na uchache wa mabasi, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi. Amesema hali hiyo ni kinyume na dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Hivyo, ameitaka UDART kuboresha haraka huduma hizo ili kuwaondolea wananchi kero wanazokumbana nazo kila siku.
Katika ziara hiyo, RC Chalamila pia ametembelea mradi wa upanuzi wa barabara ya Kimara–Ubungo unaosimamiwa na TANROADS, ambapo ametoa maagizo kwa mamlaka hiyo kuhakikisha mkandarasi anakamilisha kazi kwa wakati. Aidha, amependekeza kuwepo kwa huduma za vyoo katika vituo vikubwa vya mabasi ikiwemo Kituo cha Kimara.
Kwa upande wake, Meneja wa Upangaji Ratiba na Udhibiti kutoka UDART, Bw. Daniel Madilu, amesema tayari tathmini ya changamoto imefanyika, na mabasi mapya 100 yameshaagizwa kutoka China na yanatarajiwa kuwasili nchini mwezi Septemba mwaka huu ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Katika hatua nyingine, RC Chalamila ametembelea ofisi za DART zilizopo Ubungo Maji na kueleza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia imeweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto za usafiri wa mwendokasi. Amesema kwa mradi wa Kimara, mwekezaji mpya aitwaye Trans Dar tayari amepatikana, huku kwa barabara ya Mbagala mwekezaji aitwaye Mophat anatarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni.
Naye Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Othman Kiamia, ameahidi kushughulikia kwa haraka changamoto zilizopo kwa kuhakikisha mabasi ya kutosha na yenye ubora yanaingizwa ili kuendana na mahitaji ya wananchi, sambamba na kusimamia utoaji bora wa huduma za usafiri wa mwendokasi jijini Dar es Salaam.










