Breaking News

TANZANIA NA MISRI KUPANUA WIGO WA USHIRIKIANO

Pembezoni mwa Mkutano wa 47 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika na Mkutano wa Saba wa Uratibu wa Umoja wa Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje, Uhamiaji, na Wamisri waishio Nje wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Dkt. Badr Abdelatty.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wamejadili kwa kina mbinu za kuimarisha na kukuza ushirikiano baina ya Tanzania na Misri. Mazungumzo yao yamegusia maeneo mbalimbali ya kimkakati yanayolenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, yakiwemo kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili, kulinda mazingira na kushirikiana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia, wameangazia fursa za ushirikiano katika sekta ya anga pamoja na mpango wa kubadilishana ujuzi miongoni mwa wataalamu kutoka sekta mbalimbali. Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa ni pamoja na utalii wa mikutano na sekta ya afya, hasa katika kuimarisha miundombinu na huduma kupitia ushirikiano wa kitaalamu.

Mazungumzo haya yanaashiria dhamira ya pamoja ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kuleta maendeleo ya pande zote mbili kupitia ushirikiano wa kimkakati.