Breaking News

TANZANIA NA URUSI ZASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA UTAWALA WA KIELEKTRONIKI

Dar es Salaam - Serikali ya Tanzania na Urusi zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo saba ya utawala wa kielektroniki, kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za serikali ya Tanzania.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo kwenye Jukwaa la Kwanza la Siku Mbili la Akili Bandia (AI Forum), linalofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam. Kwa upande wa Tanzania, mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, huku Urusi ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa Centre for African Studies HSE, Bw. Andrei Maslov.
Dkt. Mwasaga amesema makubaliano hayo yanalenga kushirikiana katika maeneo saba muhimu ya utawala wa kielektroniki. Maeneo hayo ni pamoja na Kubadilishana maarifa ya utawala wa kielektroniki, Kuandaa programu za maendeleo, Kushiriki makongamano ya kitaaluma,

Ameyataja maeneo mengine kuwa ni Kubadilishana mitaala ya kielimu, Mafunzo ya kuongeza ujuzi, Kufanya tafiti za pamoja katika sekta ya TEHAMA pamoja na Kuwapa Watanzania fursa ya kwenda Urusi kujifunza masuala ya utawala wa kielektroniki.

Aidha, amesema ushirikiano huo utaimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani na kusaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kuwa kinara wa uchumi wa kidijitali barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Centre for African Studies HSE Andrei Maslov alianza kwa kuipongeza hatua hiyo na kusema makubaliano hayo yanafungua milango ya ushirikiano wa kina kati ya Tanzania na Urusi katika masuala ya TEHAMA. Ameisifu Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika mageuzi ya kidijitali na maendeleo ya teknolojia ya kisasa.

"Makubaliano hayo yanatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika matumizi ya teknolojia serikalini na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya kisasa ya utawala wa kielektroniki". Alisema Bw. Maslov.