TANZANIA YAVUTIA WAWEKEZAJI KUPITIA MAGEUZI YA SHERIA NA VIVUTIO VIPYA VYA KIUCHUMI
Dar es Salaam – Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kupitia mageuzi ya kisera na kisheria, sambamba na utoaji wa vivutio vya kiuchumi vinavyolenga kukuza uwekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Akizungumza katika Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na India lililofanyika leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), alieleza kuwa serikali imeimarisha mikakati ya kurahisisha taratibu za biashara kwa kuanzisha Sera ya Maendeleo Maalum ya Uchumi (SEDP) na kutunga Sheria Na. 6 ya mwaka 2020, ambayo huripoti moja kwa moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Kigahe, mageuzi hayo yamelenga kuimarisha usimamizi, uratibu na uendelezaji wa maeneo maalum ya kiuchumi pamoja na kuchochea utekelezaji wa bajeti ya maendeleo. Aidha, serikali imeanzisha Kituo Kimoja cha Kimataifa cha Uwekezaji (World Trade Center) kinachojumuisha zaidi ya taasisi 14 zinazohusika na utoaji wa leseni, vibali, vyeti na huduma za ufadhili wa uwekezaji.
“Kwa sasa, muda wa kushughulikia maombi ya leseni na vyeti vya uwekezaji umepunguzwa kutoka siku 14 hadi siku 7 tu za kazi. Pia tumeboresha mfumo wa utatuzi wa migogoro ya uwekezaji katika ngazi ya kimataifa,” alifafanua Kigahe.
Tanzania ni mwanachama wa mashirika na mikataba ya kimataifa inayolinda wawekezaji, ikiwemo Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA), African Trade Insurance Agency (ATI), na International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID).
Vivutio vya Kodi kwa Wawekezaji
Kupitia Tume ya Uwekezaji Tanzania (TIC), serikali inatoa vivutio vya kuvutia wawekezaji, vikiwemo:
Msamaha wa Kodi ya Mapato kwa hadi miaka 10
Msamaha wa Withholding Tax kwenye riba na gawio
Msamaha wa kodi kwenye malighafi na bidhaa adimu
Upunguzaji wa Kodi ya Mapato ya Kampuni (Corporate Tax)
Urahisi wa upatikanaji wa ardhi kwa miradi ya kimkakati
Kigahe alibainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazowavutia wawekezaji kutoka India na mataifa mengine ni pamoja na uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na India, amani na utulivu wa kisiasa, sera rafiki za biashara na idadi kubwa ya vijana wenye vipaji, elimu na nguvu kazi.
Ushirikiano wa Tanzania na India Wazidi Kuimarika
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega, alieleza kuwa ziara ya ujumbe kutoka India ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika sekta za afya, kilimo, teknolojia ya afya, na uchakataji wa mazao, ambazo India ina uzoefu na teknolojia ya hali ya juu.
Kwa mujibu wa takwimu, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka India hadi Tanzania umefikia zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 4.1 kati ya mwaka 1997 hadi Machi 2025, ukihusisha miradi 738 na ajira kwa zaidi ya watu 67,000 katika sekta kama vile utalii, viwanda, usafirishaji, afya na kilimo.
Balozi Anisa alisema kuwa Tanzania inalenga kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba kwa kushirikiana na wawekezaji wa India, kutokana na ukweli kuwa zaidi ya asilimia 85 ya bidhaa hizo bado zinaagizwa kutoka nje.
Huduma ya moja kwa moja ya ndege kati ya Mumbai na Dar es Salaam kupitia Air Tanzania, ambayo hufanyika mara nne kwa wiki, imetajwa kuwa kichocheo kingine cha kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.
Makampuni ya India Yavutiwa na Fursa Tanzania
Mwanzilishi wa taasisi ya Marketing Assistance and Research Support (MARS), Bi. Rekha Sharma, alieleza kuwa kampuni 30 kutoka India zimefika Tanzania kwa lengo la kuchunguza fursa za uwekezaji, ambapo makampuni 15 kati yao yanatoka kwenye sekta ya afya na tiba.
Kupitia ushirikiano wa MARS na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), jitihada zinafanywa kukuza uwekezaji katika sekta za afya, kilimo, viwanda na nishati mbadala.
Miongoni mwa fursa zilizovutia wawekezaji kutoka India ni:
Utengenezaji wa dawa na vifaa tiba
Uzalishaji wa malighafi za dawa (API)
Teknolojia za uchunguzi wa magonjwa (kama UKIMWI na saratani)
Madawa ya mitishamba na tiba asilia (Ayurveda)
Uanzishaji wa kiwanda cha kuchakata mafuta ya kupikia
Sekta ya magari ya umeme na vipuri
Teknolojia ya reli na vifaa vyake
Kigahe alihitimisha kwa kuwahamasisha wawekezaji kutoka India na kwingineko duniani kuchangamkia fursa lukuki zilizopo Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo limejiandaa kuwa kitovu cha biashara, viwanda na usambazaji wa bidhaa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


