TASAC YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU USALAMA WA USAFIRI MAJINI NA MCHANGO WAKE KWA UCHUMI WA TAIFA
Dar es salaam - Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema litaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama wa usafiri majini na jinsi unavyochangia katika kukuza uchumi wa taifa.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TASAC, Nahodha Mussa Mandia, alipotembelea banda la shirika hilo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Nahodha Mandia amesema kuwa TASAC lina jukumu muhimu la kudhibiti na kusimamia usalama na ulinzi wa usafirishaji kwa njia ya maji, ambao ni kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi
“TASAC inayo majukumu mawili makuu: moja ni la udhibiti, na lingine ni kuhamasisha wananchi kushiriki katika kulinda usalama wa usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji,” alisema.
Aliongeza kuwa majukumu mengine ya TASAC ni pamoja na kuhakikisha kuwa meli zote zinazotia nanga nchini kwa ajili ya kuleta bidhaa mbalimbali zinakuwa salama, sambamba na kulinda mazingira ya bahari dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na shughuli za usafirishaji majini
Kuhusu ushiriki wa shirika hilo kwenye Maonesho ya Sabasaba, Nahodha Mandia alisema TASAC linatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna linavyotekeleza majukumu yake ya kuhakikisha usalama na ulinzi wa bandari zote nchini.
Katika hatua nyingine, Nahodha Mandia alibainisha kuwa hali ya usalama katika maeneo ya baharini ni shwari, huku TASAC ikiendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama kwa shughuli zote za majini.
ok







