WAZIRI JAFO MGENI RASMI UFUNGUZI WA MAONYESHO YA PILI YA MUHARRAM EXPO JIJINI DAR
Dar es Salaam, Julai 18, 2025 – Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (BARAZA KUU) limetangaza kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maonesho ya pili ya Muharram Expo yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti Mtendaji wa Yusra Sukuk, Sheikh Mohamed Issa, amesema maonesho hayo yenye anuani “Muharram Expo” ni sehemu ya kuadhimisha mwezi wa kwanza wa Kalenda ya Kiislamu – Muharram – na yana lengo la kuhimiza huduma za kijamii na kifedha zisizo na riba.
"Kauli mbiu yetu mwaka huu ni ‘Muharram Expo: Onesha kujali jamii, toa huduma, sambaza amani’. Maonesho haya yanajumuisha huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya Sharia kama benki zisizo na riba, Vicoba, Saccos na huduma za uwekezaji Halal," alisema Sheikh Issa.
Maonesho haya pia yanalenga kutoa elimu kuhusu Masoko ya Mitaji na Dhamana, ikiwemo uwekezaji katika Hatifungani zisizo na riba (Sukuk), Mifuko ya Uwekezaji Halal (Halal Funds), na Hisa za makampuni yanayokidhi masharti ya Sharia.
Aidha, huduma za kijamii kama upimaji wa afya, utoaji wa damu salama, msaada wa kisheria na elimu ya uwekezaji wa wakfu zitapatikana kwa wageni wote watakaotembelea.
Sheikh Issa alibainisha kuwa maonesho hayo pia yamehusisha huduma za elimu kupitia vyuo vikuu vya mtandaoni, uuzaji wa vitabu vya maarifa ya Kiislamu na kijamii, pamoja na huduma kutoka taasisi za usalama kama Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Polisi. Askari wa usalama barabarani (Trafiki) pia wanatoa mafunzo na ushauri kwa waendesha bodaboda.
Kwa upande wake, Amiri wa Baraza Kuu, Sheikh Mussa Kundecha, alisema wamechagua viwanja vya wazi vya Mnazi Mmoja ili kuhakikisha wananchi wote wanapata nafasi ya kufika na kunufaika na huduma hizo bila vikwazo.
Kwa ajili ya usalama wa kiafya, gari la wagonjwa (ambulance) lipo tayari kutoa huduma za dharura kwa wanaohitaji msaada wa haraka wa kiafya.
Muharram Expo inaendelea kwa siku kadhaa zijazo huku ikitarajiwa kuvutia maelfu ya wananchi wanaotafuta huduma bora zenye kuzingatia misingi ya Kiislamu na kijamii.




