Breaking News

IRAN YAIONYA UN KUHUSU AZIMIO LA MLANGO WA HORMUZ HUKU IKISISITIZA HAKI YA KUJILINDA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameonya dhidi ya hatua yoyote ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuhusu Mlango wa Hormuz, akisema hatua hiyo inaweza kuzidisha hali badala ya kupunguza mvutano.

Katika mazungumzo ya simu siku ya Alhamisi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, viongozi hao walijadili hali ya hivi karibuni ya kikanda na kimataifa kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Araqchi alisisitiza haki ya Iran ya kujilinda kisheria ili kulinda uhuru, usalama wa taifa na mipaka yake, huku akilaani mashambulizi yaliyolenga miundombinu ya nchi hiyo, ikiwemo vyuo vikuu, madaraja na vituo vya kisayansi.

Akizungumzia hali ya usalama katika Mlango wa Hormuz, alisema imesababishwa na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel, akiongeza kuwa kwa sasa meli za nchi zisizohusika na uchokozi zinaruhusiwa kupita kwa uratibu na vikosi vya Iran.

Aidha, alikosoa juhudi za Marekani na baadhi ya nchi nyingine katika Baraza la Usalama la UN za kuweka shinikizo kwa Iran, akionya kuwa hatua zozote za uchochezi, hasa kuhusu Mlango wa Hormuz, zitaongeza matatizo badala ya kuyatatua.

Pia alilaani mashambulizi dhidi ya maeneo ya kitamaduni, ikiwemo kanisa la Orthodox mjini Tehran, akisema ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kuvitaka vyombo vya kimataifa, hususan UNESCO, kuchukua hatua.

Kwa upande wake, Lavrov alisisitiza msimamo wa Urusi wa kulaani mashambulizi dhidi ya Iran na kusisitiza umuhimu wa kurejea kwenye diplomasia ili kupunguza mvutano.

Mawaziri hao wawili walikubaliana kuendeleza mashauriano kuhusu masuala ya pande mbili, kikanda na kimataifa.