Breaking News

IZO BATTERIES KUJA NA TEKNOLOJIA YA UHIFADHI WA MAZINGIRA, AJIRA KWA WAZAWA

Dar es salaam - Kampuni ya Izo Batteries imeelezwa kuwa mfano wa uwekezaji wa kizawa unaochochea utunzaji wa mazingira na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, huku ikitoa ajira kwa Watanzania wengi kupitia shughuli za uzalishaji na usambazaji wa betri hizo.

Akizungumza kuhusu ubora wa bidhaa hizo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Izo Mahenge amesema kiwanda hicho kinazingatia viwango vya kisasa vya uzalishaji vinavyolenga kulinda mazingira, ikiwemo matumizi ya teknolojia isiyotumia maji kwenye betri hizo, jambo ambalo linapunguza athari za uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wake, balozi wa bidhaa hizo, Doto Magari amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wazawa kwa kuboresha miundombinu na kuruhusu viwanda vya ndani kustawi, hali inayochangia kuongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi.

Alisema uwekezaji wa viwanda vya ndani unasaidia vijana kupata ajira na kujifunza ujuzi wa kazi za viwandani, huku akiwahimiza Watanzania kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini ili kukuza uchumi wa taifa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa bora barani Afrika.