Breaking News

BODI YA BIMA YA AMANA YAHIMIZA WANANCHI KUTUNZA FEDHA BENKI

GEITA - Bodi ya Bima ya Amana imewataka wananchi kuweka fedha zao katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania badala ya kuzitunza majumbani, ili kupunguza hatari ya kupotea kutokana na wizi, moto na changamoto nyingine.

Rai hiyo imetolewa na Afisa kutoka Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Bodi ya Bima ya Amana, Pius Makulilo, wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Zanzui pamoja na waandishi wa habari waliotembelea banda la Bodi hiyo katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.

Makulilo amesema wanafunzi hao wamepewa elimu kuhusu Bodi ya Bima ya Amana, majukumu yake pamoja na umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha, huku wakitakiwa kuwa mabalozi kwa wazazi wao katika kuhamasisha utunzaji salama wa fedha.

Amesema fedha zinazotunzwa majumbani zinaweza kupotea kwa sababu mbalimbali, ikiwemo moto, wizi au kuharibiwa na mchwa, tofauti na fedha zinazowekwa katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ambazo zinakuwa chini ya mfumo wa Bima ya Amana kwa mujibu wa sheria na taratibu.

"Sehemu sahihi ya kutunza fedha ni kwenye benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu, siyo kutunza fedha ndani,” amesema Makulilo.
Aidha, Makulilo amefafanua kuwa mteja hahitajiki kujiunga moja kwa moja na Bodi ya Bima ya Amana. Amesema mtu anapofungua akaunti katika benki yenye leseni ya Benki Kuu, amana yake huingia katika mfumo wa Bima ya Amana kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Katika ziara hiyo, wanafunzi na walimu waliuliza maswali mbalimbali, likiwemo namna ya kujiunga na Bodi ya Bima ya Amana, mahali ofisi zake zilipo na kinachotokea endapo mteja mwenye fedha katika benki atafariki.

Kuhusu mrithi wa fedha, Makulilo amesema wakati wa kufungua akaunti mteja huweka taarifa za mtu wa karibu au mrithi, ikiwemo jina na mawasiliano yake. Hata hivyo, katika tukio la kifo, taratibu za kupata fedha hufuata matakwa ya kisheria na nyaraka zinazothibitisha uhalali wa mrithi.

Amesema makao makuu ya Bodi ya Bima ya Amana yapo Dodoma, huku ikiwa na ofisi pia katika majengo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Makulilo amesema elimu hiyo imetolewa katika maonesho hayo kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi, hususan wanafunzi na wazazi wao, kuhusu umuhimu wa kutumia taasisi rasmi za kifedha na usalama wa amana zao.