Breaking News

KIJANI CONCERT WATOA ELIMU YA MBEGU BORA KWA WAKULIMA GEITA

GEITA - Taasisi ya Kijani Concert Tanzania imefungua fursa kwa wakulima mkoani Geita kupata mbegu bora zinazohimili ukame na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, sambamba na elimu ya matumizi sahihi ya mbegu na kanuni bora za kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kijani Concert Tanzania, Mandalin Kahindi, amesema taasisi hiyo pia inatekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuwawezesha wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza tija katika kilimo.

Kahindi amesema Kijani Concert inasambaza mbegu za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo ukanda wa Magharibi na Mashariki, zikiwemo mbegu za mahindi, mpunga na mazao ya mboga mboga.

Amesema mbegu hizo zina uwezo wa kuhimili ukame na kusaidia wakulima kupata mavuno yenye tija, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni bora za kilimo kulingana na mazingira ya eneo husika.

“Pamoja na kuwapa mbegu bora, tunawapa pia elimu ya namna ya kuzitumia na kufuata kanuni bora za kilimo ili waweze kupata mavuno yaliyo bora,” amesema Kahindi.

Amesema ushiriki wa taasisi hiyo katika Maonesho ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan mkoani Geita unatokana na umuhimu wa kilimo katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na kuchangia shughuli nyingine za kiuchumi.

Amesema shughuli za madini haziwezi kutenganishwa na umuhimu wa uzalishaji wa chakula, hivyo elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbegu bora ni sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji.

Kahindi amewataka wakulima kuepuka kulima katika maeneo hatarishi, ikiwemo mabondeni wakati wa vipindi vya mvua nyingi, pamoja na kuzingatia mwelekeo wa maji wakati wa kuandaa mashamba.
Kwa upande wake, Bi. Matrida Philipo kutoka Kijani Concert Tanzania, amesema taasisi hiyo inashiriki maonesho hayo ikiwa na mbegu mbalimbali zinazozalishwa na Wakala wa Mbegu Tanzania, huku akiwataka wakulima kutembelea banda lao kupata mbegu na elimu ya kilimo.

Amesema miongoni mwa mbegu zinazopatikana ni mahindi aina ya TMA 115, ambayo hukomaa kwa takribani siku 113 na inapatikana katika kifungashio cha kilo mbili.

Amesema pia kuna mbegu ya mahindi ya muda mfupi inayokomaa ndani ya siku 75, pamoja na mbegu ya mpunga aina ya SARO inayopatikana katika kifungashio cha kilo tano.

Aidha, amesema Kijani Concert inapatikana na mbegu mbalimbali za mboga mboga na inatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbegu hizo ili kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji.

“Tunawakaribisha wakulima wote wafike katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan wapate elimu na mbegu bora. Zaidi ya mbegu, tunatoa pia elimu kuhusu namna ya kuzitumia na kufuata kanuni bora za kilimo,” alisema Bi Matrida