WAZIRI SANGU AITAKA WCF KUHARAKISHA FIDIA NA KUONGEZA ELIMU KWA WAFANYAKAZI
GEITA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, ameitaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuongeza elimu kwa wafanyakazi kuhusu haki zao za fidia na kuendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuhakikisha madai yanashughulikiwa kwa wakati.
Sangu alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza katika banda la WCF wakati wa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita, akisisitiza umuhimu wa WCF katika kuwalinda wafanyakazi wanaopata ajali, magonjwa au majanga yanayohusiana na kazi.
Alisema sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania, ikichangia takribani asilimia 10.1 ya Pato la Taifa na kuajiri idadi kubwa ya Watanzania, hali inayofanya uwepo wa mfumo madhubuti wa fidia kuwa muhimu kwa wafanyakazi na wategemezi wao.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, WCF imeendelea kuimarika katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo kuboresha mifumo ya TEHAMA inayowezesha uwasilishaji na ushughulikiaji wa madai na malalamiko ya wafanyakazi.
Sangu alisema mfuko huo kwa sasa una thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.1, kutoka takribani Sh bilioni 770, akieleza kuwa ukuaji huo umeongezeka kwa kasi katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ni wito kwa wafanyakazi wote ambao wanapata changamoto wasiwe na wasiwasi. WCF imejitabainisha kwa kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA,” alisema Sangu.
Aidha, aliwataka waajiri ambao bado hawajajiunga na WCF kuhakikisha wanafanya hivyo ili kuwawezesha wafanyakazi wao kupata haki ya fidia endapo watapata ajali, majanga au changamoto nyingine zinazohusiana na kazi.
Sangu pia aliitaka WCF kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi, hususan katika sekta ya madini, ili waweze kufahamu haki zao, taratibu za kudai fidia na hatua za kuchukua wanapopatwa na majanga kazini.
Alisema elimu hiyo ni muhimu katika kupunguza malalamiko na kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma za mfuko huo kwa ufanisi na kwa wakati.
Waziri huyo aliipongeza WCF kwa kushiriki katika maonesho hayo na kwa hatua ilizochukua katika kutoa elimu kwa wafanyakazi wa sekta ya madini, akisema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali na kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




