WAZIRI SANGU AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO KUJIUNGA NA HIFADHI SCHEME
GEITA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, amewataka wachimbaji wadogo nchini kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia Hifadhi Scheme ili kujilinda dhidi ya athari za majanga na changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya kupoteza uwezo wa kufanya kazi.
Sangu ametoa wito huo mkoani Geita wakati akizungumza katika banda la NSSF kwenye Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani humo, akisema wachimbaji wadogo ni miongoni mwa makundi yanayolengwa na mpango huo kutokana na aina ya shughuli wanazofanya.
Amesema Hifadhi Scheme inalenga watu waliojiajiri ambao awali hawakuwa na mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii, wakiwemo mama na baba lishe, waendesha bodaboda pamoja na wachimbaji wadogo.
Kwa mujibu wa Sangu, watu wanaojiajiri wanaweza kuwa na uwezo wa kufanya kazi na kupata kipato leo, lakini wanaweza kukumbwa na majanga au kushindwa kuendelea na shughuli zao siku zijazo, hivyo wanahitaji kuwa na mfumo wa kuwasaidia wakati wa changamoto.
“Leo ana nguvu ya kufanya kazi, leo ana nguvu ya kuwa mgodini, lakini kesho anaweza kupata majanga. Atakayekuwa kimbilio lake ni NSSF kupitia Hifadhi Scheme,” amesema.
Sangu pia ameipongeza NSSF kwa kushiriki katika maonesho hayo, akisema ushiriki huo unaonesha namna mfuko huo unavyotambua umuhimu wa sekta binafsi na sekta ya madini katika uchumi wa nchi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema katika utekelezaji wa dira hiyo, sekta binafsi inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa, huku NSSF ikiwa na nafasi ya kuhakikisha wafanyakazi na watu waliojiajiri wanapata ulinzi wa kijamii.
Aidha, Sangu amesema NSSF imeweka mpango wa kukuza thamani ya mfuko hadi kufikia Sh trilioni 24 ifikapo mwaka 2031, akieleza kuwa thamani ya mfuko imeongezeka kutoka Sh trilioni 5.7 mwaka 2022 hadi Sh trilioni 10.4 Desemba mwaka jana.
Amesema kwa sasa thamani ya mfuko imefikia Sh trilioni 11.5 na inatarajiwa kufikia zaidi ya Sh trilioni 12 ifikapo Desemba mwaka huu.
Kwa upande wake, mwakilishi wa NSSF amesema ofisi hiyo mkoani Geita imeweka mkakati wa kuwafikia watu waliojiajiri, wakiwemo waendesha bodaboda, mama na baba lishe pamoja na wachimbaji wadogo, kwa kushirikiana na viongozi wa makundi hayo.
Amesema kwa mwaka wa fedha uliopo, NSSF Geita imepewa lengo la kuandikisha wanachama 5,674 kutoka kundi la waliojiajiri na tayari imefikia asilimia 50 ya lengo hilo katika kipindi cha miezi tisa.
Ameongeza kuwa NSSF inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya madini, ikiwemo kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), katika utekelezaji wa mifumo ya ziada ya hifadhi ya jamii.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, NSSF imejiwekea lengo la kukusanya Sh bilioni 9.1 kutoka kwenye sekta ya watu waliojiajiri na kupitia mpango wa hifadhi ya ziada katika mwaka huu wa fedha.
Amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha watu wanaojiajiri, hususan wale wanaofanya shughuli zenye changamoto kama uchimbaji mdogo wa madini, wanakuwa na ulinzi wa kijamii wakati wa majanga au wanapofikia hatua ya kushindwa kuendelea na shughuli zao.




