ZIMAMOTO WATOA MUONGOZO KUKABILIANA NA EL NINO
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limewataka wananchi, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali kuchukua tahadhari na kufanya maandalizi mapema ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua za Vuli na hali ya El Niño inayotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba mwaka huu.
Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Naibu Kamishna Puyo Nzalayaimisi, amesema maandalizi ya mapema ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo na hali hiyo ya hewa.
Amesema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko na kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya mamlaka husika wakati wote wa msimu wa mvua.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwa makini zaidi na watoto ili kuwakinga dhidi ya maeneo hatarishi, huku akizitaka taasisi zinazohusika kuondoa vizuizi vinavyoweza kuzuia mtiririko wa maji na kuongeza hatari ya mafuriko.
Naibu Kamishna Nzalayaimisi pia amewataka wasafirishaji wa nchi kavu na majini kuongeza umakini katika shughuli zao, hususan wakati wa mvua, ili kupunguza uwezekano wa ajali na madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, Serikali, sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha hatua za kinga na uokoaji zinachukuliwa kwa wakati.




