GGM YAONESHA TEKNOLOJIA ZA UCHIMBAJI KWA WASHIRIKI WA MAONESHO YA MADINI
GEITA - Washiriki wa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa leo Oktoba 1, 2026, wametembelea Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), mkoani Geita, kwa lengo la kujifunza na kuona kwa vitendo shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuhakikisha uzalishaji na usalama wa wafanyakazi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mining Superintendent wa Open Pit Mining katika GGM, Jeffex, amesema washiriki hao wametembelea eneo la Nyankanga Pit, ambalo ni eneo la kihistoria la mgodi huo lililoanza shughuli za uchimbaji mwaka 1999.
Amesema Nyankanga ilianza kama mgodi wa wazi (open pit), lakini baada ya kina cha madini kufika hatua ambayo uchimbaji wa wazi ukawa na changamoto zaidi, shughuli zilihamishiwa katika mfumo wa uchimbaji wa chini ya ardhi (underground mining).
Kwa mujibu wa Jeffex, GGM kwa sasa inaendesha aina zote mbili za uchimbaji, huku baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakichimbwa kwa mfumo wa open pit yakihamishiwa underground, ikiwemo Nyankanga, Star & Comet na Geita Hill.
Amesema uchimbaji wa underground una gharama kubwa zaidi za uendeshaji ikilinganishwa na open pit, huku open pit ukihitaji kuondoa kiasi kikubwa cha udongo na miamba isiyo na madini (waste) ili kufikia tabaka lenye dhahabu.
Akizungumzia usalama, Jeffex amesema GGM inatumia teknolojia mbalimbali ikiwemo radar za ufuatiliaji wa kuta za migodi, kamera na mifumo ya kufuatilia hali ya waendeshaji wa mitambo, ili kubaini mapema viashiria vya hatari na kuchukua hatua kabla ya ajali kutokea
Amesema pia mgodi umejiandaa kukabiliana na changamoto za mvua kubwa kwa kuweka mifereji ya kuzuia maji kuingia kwenye mashimo ya uchimbaji pamoja na pampu za kusukuma maji, ili shughuli za uzalishaji ziendelee.
Kwa upande wake, mfanyakazi na opereta wa GGM, Khadija Adamu, amesema alipata mafunzo ya kuendesha malori makubwa ya uchimbaji kupitia mfumo wa simulator kabla ya kuruhusiwa kuendesha mitambo hiyo katika mazingira halisi ya mgodi.
Khadija amesema mafunzo hayo yalichukua takribani miezi mitatu, na kwamba mfumo huo unamwezesha mwendeshaji kujifunza namna ya kuendesha mashine na kukabiliana na mazingira mbalimbali kabla ya kupewa jukumu la kuendesha mtambo halisi.
Amesema kufanya kazi katika sekta ya madini kumemsaidia kutimiza ndoto yake huku akieleza kuwa GGM imeendelea kutoa nafasi kwa wanawake kushiriki katika kazi zinazohusisha uendeshaji wa mitambo mikubwa.
Khadija pia amesisitiza umuhimu wa usalama kazini, akieleza kuwa kabla ya kuanza kazi wafanyakazi hutumia mfumo wa “Take 5”, unaowataka kusimama na kutafakari, kutambua viatarishi, kudhibiti hatari, kutoa taarifa kwa wengine na kisha kuendelea na kazi kwa usalama.
Ametoa wito kwa wanawake ambao wana ndoto ya kufanya kazi katika sekta ya madini kutokubali kukatishwa tamaa na mitazamo kwamba baadhi ya kazi ni za wanaume pekee.
Amesema wanawake wana uwezo wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za sekta ya madini endapo watapata fursa, mafunzo na kujiamini katika kutekeleza majukumu yao.
Ziara hiyo imewapa washiriki wa maonesho hayo fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu mifumo ya uchimbaji wa wazi na wa chini ya ardhi, matumizi ya mitambo mikubwa, teknolojia za usalama na nafasi ya wanawake katika sekta ya madini.









