Breaking News

TTCL YAFUNGA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA, YASISITIZA HUDUMA BORA

DAR ES SALAAM – Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limehitimisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka 2026 kwa kusisitiza umuhimu wa wafanyakazi kuongeza juhudi katika kuwahudumia wateja, kutatua changamoto zao kwa haraka na kuboresha uzoefu wao wa kupata huduma za mawasiliano.

Akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa TTCL, Diwan Mwamengo, amesema kauli mbiu ya mwaka huu, “The Extra Mile” (Hatua ya Ziada kwa Mteja), inawataka wafanyakazi kwenda zaidi ya majukumu yao ya kawaida ili kuhakikisha wateja wanasikilizwa, wanathaminiwa na kupata ufumbuzi wa changamoto zao kwa wakati.

Mwamengo amesema utoaji wa huduma bora unahitaji wafanyakazi kufuatilia malalamiko hadi yanapotatuliwa, kutoa taarifa sahihi kwa wakati, kushirikiana kati ya idara na kutumia ubunifu na teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Amesisitiza kuwa huduma kwa wateja si jukumu la kitengo kimoja pekee, bali ni wajibu wa kila mfanyakazi wa TTCL, akibainisha kuwa ubora wa huduma ndio msingi wa kujenga uaminifu kwa wateja na kuongeza ushindani wa shirika katika soko la mawasiliano.

Amesema TTCL inaendelea kuimarisha huduma zake za mawasiliano na suluhisho za kidijitali, ikiwemo Fiber Mlangoni Kwako, huduma za simu, intaneti na Public Wi-Fi, huku akiwataka wafanyakazi kuhakikisha uwekezaji huo unaendana na huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Mnandwa Mnandwa, amesema huduma ya Public Wi-Fi inayotolewa na TTCL imewanufaisha wanafunzi kwa kuwapa fursa pana ya kupata intaneti kwa ajili ya shughuli zao.
Mnandwa amesema ushirikiano kati ya wanafunzi na TTCL umekuwa mzuri, hasa katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza, na kuongeza kuwa wanafunzi wamekuwa wakiitumia na kuitangaza huduma hiyo kutokana na manufaa wanayoyapata.

Ameishukuru menejimenti ya TTCL kwa huduma hiyo na kuiomba kuendelea kuiboresha ili iendelee kukidhi mahitaji ya wanafunzi.

Nao wateja Huruma, mkazi wa Mombasa, Ukonga, na Rajabu, mkazi wa Kariakoo, wameeleza kunufaika na huduma mbalimbali za TTCL, zikiwemo huduma za simu, Fiber Mlangoni Kwako na Public Wi-Fi inayopatikana katika maeneo ya wazi, vituo vya usafiri na vyuoni.
Maadhimisho hayo yamelenga kuimarisha mahusiano kati ya TTCL na wateja wake, kusikiliza maoni yao na kuhamasisha utamaduni wa utoaji wa huduma bora unaozingatia mahitaji ya wateja.

Akihitimisha hafla hiyo, Mwamengo ametangaza rasmi kufungwa kwa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka 2026, akisisitiza kuwa kufungwa kwa wiki hiyo si mwisho wa dhamira ya shirika katika kuboresha huduma, bali ni mwanzo wa kutekeleza kwa vitendo ahadi ya kuwahudumia wateja kwa ufanisi zaidi.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa: “The Extra Mile” Huduma bora, hatua ya ziada kwa mteja.