Breaking News

TTCL YAZINDUA MSIMU WA BURE, KUTOA VIFAA KWA WATEJA WA FIBER

Dar es salaam - SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua kampeni ya msimu wa bure kwa wateja wa huduma ya Fiber Mlangoni Kwako, inayolenga kuwawezesha Watanzania kupata huduma za intaneti na mawasiliano kwa gharama nafuu katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

Kupitia kampeni hiyo, wateja wapya na waliopo watakaolipia kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi watanufaika na vifaa na huduma mbalimbali bila gharama za ziada, ikiwemo simu ya mezani, ruta (router), laini tatu za simu na huduma ya burudani ya T-Burudani.

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, alisema hatua hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kuendelea kuwasiliana na kutumia intaneti kwa urahisi, hususan katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Alisema huduma ya Fiber Mlangoni Kwako imekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka miwili, ikihudumia makundi mbalimbali ya wateja, yakiwemo familia, wafanyabiashara wadogo na maeneo yenye shughuli za kijamii.

Mwita alisema TTCL imeendelea kuboresha huduma hizo kwa kutumia teknolojia mbalimbali kulingana na mabadiliko ya teknolojia duniani, ambapo kwa sasa inatumia teknolojia ya kisasa ya XGPON.
Alisema TTCL imekuwa ikitoa huduma ya Fiber Mlangoni Kwako kwa zaidi ya miaka miwili, ikihudumia familia, wafanyabiashara wadogo na maeneo mbalimbali yenye shughuli za kijamii.

Aliongeza kuwa shirika hilo linaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo XGPON, huku likitekeleza awamu ya pili ya mradi wa Fiber Mlangoni Kwako katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, wateja watakaojiunga na kifurushi cha Triple Hub cha Shilingi 70,000 au zaidi watapatiwa simu ya mezani inayounganishwa na ruta, pamoja na laini tatu zitakazowawezesha kutumia intaneti ya kifurushi chao wanapokuwa maeneo mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa kampeni hiyo imekuja katika kipindi ambacho familia nyingi hukutana nyumbani kutokana na likizo za mwisho wa mwaka na kufungwa kwa shule, hivyo kuongeza umuhimu wa huduma bora za intaneti katika mawasiliano na burudani.

“Tunafahamu kuwa wateja wetu wanahitaji huduma zinazowawezesha kuendelea kuwasiliana wanapokuwa nyumbani na hata wanapokuwa nje ya nyumba zao. Ndiyo maana tumekuja na kifurushi cha Triple Hub kinachowawezesha kufurahia huduma hizo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwita, mteja atakayejiunga na kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi atapatiwa simu ya mezani na ruta bila malipo, huku simu hiyo ikiunganishwa moja kwa moja kwenye ruta ili kumwezesha kupiga simu kwa mujibu wa masharti ya kifurushi chake.

Aidha, mteja huyo atapewa laini tatu za simu zitakazomwezesha yeye na wanafamilia kutumia huduma za intaneti kupitia simu za mkononi wakiwa maeneo mbalimbali nchini Tanzania, kwa mujibu wa masharti ya huduma hiyo.
Alisema wateja hao pia wataunganishwa na huduma ya T-Burudani, inayowawezesha kutazama filamu, tamthilia na maudhui mengine ya burudani.

Mwita alisema wateja wapya wanachotakiwa kufanya ni kujaza fomu za kuomba huduma ya Fiber Mlangoni Kwako na kuchagua kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi. Baada ya kukamilisha taratibu hizo, timu ya TTCL itafika kuwaunganishia huduma pamoja na kuwapatia vifaa vilivyoainishwa kwenye kampeni hiyo.

Kwa upande wa wateja waliopo, alisema wale wanaotumia kifurushi cha Sh 55,000 wanaweza kunufaika na ofa hiyo kwa kuboresha vifurushi vyao kwenda Triple Hub ya Sh 70,000 au zaidi.

Aliongeza kuwa wateja hao wanapaswa kufika katika ofisi au maduka ya TTCL yaliyo karibu nao wakiwa na namba zao za huduma (service number) ili kuhakikiwa na kupatiwa vifaa na huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.
Alisema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kupanua matumizi ya intaneti na kuwawezesha wateja kutumia huduma zao za nyumbani hata wanapokuwa safarini au katika maeneo mengine.

Mwita alibainisha kuwa huduma hiyo itapatikana katika maeneo ambayo TTCL imeweka miundombinu ya Fiber Mlangoni Kwako, yakiwemo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa na Unguja, Zanzibar.

Aliwahimiza Watanzania wanaoishi katika maeneo yenye huduma hiyo kutembelea ofisi na maduka ya TTCL ili kupata maelezo zaidi na kujiunga na kifurushi kinachowawezesha kunufaika na ofa hiyo.

Alisema kupitia kampeni hiyo, wateja wataweza kutumia intaneti ya nyumbani na kuendelea kuwasiliana na familia zao wakiwa katika maeneo mbalimbali, bila kulazimika kutegemea vifurushi tofauti vya intaneti kila wanapokuwa nje ya nyumba zao, kwa kuzingatia masharti ya huduma husika.