MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WA MWEZI JULAI 2016 UMEPUNGUA HADI ASILIMIA 5.1.
Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraimu Kwesigabo
(kulia) akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai, 2016 ambao umefikia
asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5 za mwezi Juni 2016.Kushoto ni Kaimu Meneja wa
wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth
Minja.
Baadhi
ya waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Mwezi Julai,
2016 iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Ephraimu Kwesigabo leo jijini Dar es salaam. Picha/Aron
Msigwa –MAELEZO.
Na.
Aron Msigwa –MAELEZO
OFISI
YA TAIFA YA TAKWIMU (NBS) imetangaza mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai
2016 na kueleza kuwa umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5
iliyokuwepo mwezi Juni mwaka huu.
Akitangaza
taarifa ya mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai, 2016 leo jijini Dar es
salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw.
Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa
mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo
kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2016.
Ameeleza
kuwa kupungua kwa mfumuko wa Bei wa mwezi Julai 2016 kumechangiwa na kupungua
kwa kasi ya bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na zile zisizo za vyakula kwa
kipindi kilichoishia Julai 2016 zikiwemo bidhaa za samaki kwa asilimia 6.6,
mafuta ya kupikia asilimia 4.9 na maharage kwa asilimia 1.9 huku bei zisizo za
vyakula zikihusisha ni gesi kwa asilimia
21.5, mafuta ya taa 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua bei ni pamoja na
bidhaa za gesi kwa asilimia 21.5, mafuta ya taa kwa asilimia 9.4 na dizeli kwa
asilimia 10.3.
Aidha,
ameeleza kuwa pamoja kupungua huko, kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma
kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 kwenye baadhi ya bidhaa umeonesha kuongezeka
katika kipindi hicho hasa kwenye kama mchele,
mahindi, unga wa mahindi, vyakula kwenye migahawa na mkaa.
Bw.
Kwesigabo amesema kuwa Fahirisi za Bei nazo zimeongezeka hadi kufikia 103.50
mwezi Julai, 2016 kutoka 103.47 za mwezi Juni 2016, ongezeko ambalo limechangiwa na kuongezeka kwa bei ya
baadhi ya bidhaa za vyakula zile zisizokuwa
za vyakula.
Amesema
ongezeko hilo la Fahirisi linahusisha kundi la bidhaa na huduma za vyakula na
vinywaji baridi, Vinywaji vyenye kilevi na bidhaa za Tumbaku, Mavazi ya nguo na
viatu, nishati, maji na Makazi pamoja na Samani, vifaa vya nyumbani na
ukarabati wa nyumba.
Kundi
lingine linahusisha gharama za Afya, usafirishaji, Mawasiliano, Utamaduni na
Burudani, Elimu, hoteli na migahawa pamoja na bidhaa na huduma nyinginezo ambazo
jumla ya Fahirisi za Bidhaa hizo kwa mwezi huo zimefikia 103.50.
“Baadhi
ya bidhaa zilizo sababisha kuongezeka kwa Fahirisi ni pamoja na mafuta ya
kupikia asilimia 1.1, samaki wabichi asilimia 6.0, matunda asilimia 4.9,
maharage makavu kwa asilimia 2.7, ndizi za kupika asilimia 1.9 na mahindi kwa
asilimia 1.5” Amesisitiza Kwesigabo.
Mbali
na hilo ameeleza kuwa Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za vyakula na vinywaji baridi
kwa mwezi Julai 2016 umepungua hadi kufikia asilimia 7.6 kutoka asilimia 8.1 ya
mwezi Juni 2016.
Kwa
upande wa uwezo wa shilingi ya 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma
umefikia shilingi 96 na senti 62 mwezi Julai 2016 ikilinganishwa na shilingi 96
na senti 65 ya mwezi Juni, 2016.
Aidha,
hali ya Mfumuko wa Bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki imeonesha kuwa
nchi ya Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Julai umeongezeka hadi kufikia asilimia
6.39 kutoka asilimia 5.80 za mwezi Juni, 2016, Uganda ikiwa na Mfumuko wa Bei
uliopungua wa asilimia 5.1 kwa mwezi Julai kutoka asilimia 5.9 za mwezi Juni,
2016.





