STARTIMES YACHANGIA MADAWATI MKOANI MTWARA
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura
(kushoto) pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura
Hanif (kulia) wakiwa kwenye baadhi ya madawati yaliyochangiwa na kampuni
hiyo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati
nchi nzima iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.
Dkt. John Pombe Magufuli. Zoezi hio la uchangiaji wa madawati
lilifanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mwishoni mwa wiki
hii.
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura
(kushoto) pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura
Hanif (kulia) wakiwa wamekaa kwenye madawati hayo.
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura
(kulia) , akizungumza wakati wa kupokea madawati hayo. Katikati ni Mkuu
wa Wilaya ya Mtwara, Mh. Dkt. Khatib Malimi Kazungu
Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kushoto), akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo.
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura
amepokea madawati hamsini yenye thamani ya shilingi milioni tano kutoka
kwa kampuni ya matangazo ya dijitali ya StarTimes ikiwa ni jitihada za
kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati iliyoanzishwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli.
Akizungumza
mara baada ya hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki
moani Mtwara, Mh. Bi. Wambura amebainisha kuwa zoezi la kuchangia
madawati ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri
linawahusu watu wote na sio serikali pekee.
“Ningependa
kuchukua fursa hii kuzipongeza taasisi za umma na sekta binafsi kwa
mwitikio wao mkubwa wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika kampeni ya
kuchangia madawati. Wote tunafahamu ni kwa kiasi gani shule nyingi
nchini zinavyokabiliwa na uhaba wa madawati jambo linalopelekea
mazingira magumu ya kufundishia na kujinzia.
Lakini kwangu mimi suala la
wanafunzi kuongezeka sioni kama ni tatizo bali ni changamoto kwa
serikali yetu na jamii kwa ujumla kuendana na mwamko mkubwa wa wazazi na
walezi kuwapeleka watoto wao shule. Kwa muda mrefu sana serikali
imekuwa ikiwahamasisha wananchi wake wawapeleke watoto shule na
wakafanya hivyo, sasa suala hilo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa na vivyo
jinsi walivyoitikia mwamko huo basi waitikie na wa huu wa kuchangia
madawati.” Alisema Mh. Bi. Wambura.
Naibu
Waziri huyo aliendelea kwa kuelezea kuwa serikali ina wajibu wa
kuhamasisha maendelea kwa wananchi wake kwa njia mbalimbali ikiwemo hii
ya kuwasilisha maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kama vile suala
la elimu nchini.
“Elimu
ndio suala la msingi katika taifa lolote duniani iwe lililoendelea au
linaloendelea na ndio maana kwa nchi za wenzetu wanawekeza fedha nyingi
katika sekta hii.
Nchi yoyote yenye wasomi wengi lazima itakuwa na
maendeleo makubwa kutokana na raia wake kuelimika lakini hayo yote haya
hayatowezekana kama tusipowawekea mazingira mazuri wanafunzi wetu tangu
ngazi ya msingi,” alisema Mh. Naibu Waziri na kumalizia, “Ningependa
kumalizia kwa kuwapongeza na kuwashukuru wenzetu wa kampuni ya StarTimes
kwa kuguswa na suala hili na kuamua kuja huku Mtwara kuchangia madawati
kwani huku ndiko kwenye changamoto kubwa hasa kutokana na taasisi na
makampuni mengi kuwepo sehemu za mijini.
Tunawashukuru sana na
tunawaomba muendelee na moyo huo huo na mfike sehemu nyingine amabko
makampuni mengine hayafiki.”
Kwa
upande wake Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif
amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ni mdau mkubwa wa masuala ya kijamii
hususani elimu kwa inafahamu umuhimu wake katika kuleta mapinduzi ya
kimaendeleo.
“StarTimes
ni mdau mkubwa sana wa masuala ya elimu na kwa muda mrefu tumekuwa
tukisaidia shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Uchangiaji wa
madawati ni kampeni ya aina yake iliyoanzishwa na Mh. Rais Magufuli na
inahitaji kuungwa mkono kwa nguvu zote kwani yeye aliamini kabisa
watanzania tunao uwezo huo ila tulikosa tu uhamasishaji.
Na ni kweli
uhamasishaji ndio uliokosekana kwani mara baada ya kutoa tamko hilo
taasisi, makampuni, mashirikia, wananchi na watu binafsi wameonyesha
mwitikio mkubwa. Hii ni dalili njema kwamba watanzania tunaweza kuleta
maendeleo yetu wenyewe bila ya kungojea msaada kutoka kwa watu wa nje.”
Alisema Bi. Hanif
“Leo hii
tumekuja huku Mtwara kuja kukabidhi madawati haya, tunafahamu kwamba ni
machache lakini yatakuwa ni msaada mkubwa kwa watoto wetu kusoma katika
mazingira mazuri. Wanafunzi wanaposoma katika mazingira mazuri hupelekea
kuhudhuria vipindi, kuipenda shule, kuelewa vizuri na hatimaye
kupelekea kufaulu masomo yao,
” alisema na kuhitimisha Bi. Hanif kuwa,
“Wananfunzi wanapowekewa mazingira mazuri ya kusomea pia hutoa hamasa
kwa walimu kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa kwani ufundishaji unakuwa
ni rahisi na vivyo hivyo uelewa kwa wanafunzi.
Hivyo basi, ningependa
kutoa wito kwa wanafunzi wayatunze madawati haya ili yaje kuwanufaisha
na wenzao watakaokuja siku za usoni na tunawaahidi kuwa tuko pamoja nao
katika kutatua changamoto zinazowakabili.”



