Breaking News

DC ILALA ATOA MAAGIZO MAZITO URASIMISHAJI ARDHI

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, ameeleza kuchoshwa na  malalamiko ya wananchi juu ya kudaiwa kutapeliwa na kampuni zinazohusika na urasmishaji ardhi na kuyataka makampuni yaliyoshindwa kufanya kazi hiyo kujiondoa.

Ameonya,  kampuni yoyote ya ardhi iliyopewa  kazi hiyo ambayo  mmiliki wake atashindwa kuwasilisha taarifa kwa wanachi, kuto kuhudhuria vikao na kuitikia wito  atakamatwa na polisi.

Aliyasema hayo Dar es Salam,leo  katika kikao kilicho husisha,  wakandarasi wa urasimishaji ardhi, wenye viti wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na mitaa, maofisa ardhi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na mkoa huo pamoja na wenyeviti wa kamati za urasmishaji ardhi  za mitaa.

Ludigija, alisema anasikitishwa na malalamiko mengi anayoendelea kupokea kutoka kwa wananchi juu ya migogoro ya ardhi hasa urasimishaji huo, ambapo wengi wanalalamikia makampuni yaliyopewa kazi hiyo kuchukua fedha na kuingia mitini.

“Nimechoshwa na malalamiko ya migogoro ya ardhi hasa katika urasimishaji. Kama kuna kampuni ambayo ilipewa  kazi hiyo na wananchi kupima mitaa yao na  inaona imeshindwa kuendelea na urasimishaji ijiondoe ili kazi hiyo ifanywe na watu wengine,”alisema.

Pia mkuu huyo wa wilaya alitaka kampuni zote  zillizopewa  kazi hiyo kuhuisha mikataba yao  ya urasimishaji ardhi waliyosainisha na wananchi kwani mingi imekwisha muda wake.

“Ninatoa siku  saba wahusika  wote waripoti  Juni 13 asubuhi katika kikao kitakachofanyia  katika ukumbi wa Arnatoglou kitakacho hususha wadau wote,”alieleza Ludigija.

Alisema yapo makampuni 50 ya urasimishaji ardhi yanayofanya kazi wilayani humo lakini  asilimia kubwa yanalalamikiwa na wananchi kwa kushindwa  kutekeleza wajibu wao.

Ludigija aliagiza wenye viti wa serikali za mita kuitisha  mkikutano ya  wananchi katika maeneo yao na kuwapa taarifa sahihi za namna ya zoezi la urasimishaji linavyoendelea.

Alisema, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inataka kila kipande cha ardhi kina pimwa, ili wananchi watumie nyumba  na ardhi yao kufanya shughuli za maendeleo, ikiwemo kupata mikopo.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya alionya, wananchi ambao hawatarasimisha ardhi kwa makusudi,  serikali wilayani humo haitasikiliza migogoro yao inayo husu ardhi na badala yake waende moja kwa moja mahakamani.

“Wapo wanaoona urasimishaji ardhi ni hiyari. Hawatoi fedha za kurasimisha ardhi yao. Tukimaliza urasimishaji huu  kama kuna mwananchi atakuwa ameshindwa kurasimisha eneo lake asije ofisini kwangu. Sitashughulikia mgogoro wake,”

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salam,  Tabu Shaibu, alikili kuwepo kwa changamoto za aardhi na kueleza kuwa serikali  itashughulikia kikamilifu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao.

Kaimu  Kamishna  wa  Ardhi Msaidizi wa  Mkoa wa Dar es Salam, Idrisa Kayera, alisema ipo changamoto  ya elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu urasimishaji ardhi  na wengi kushindwa kutoa fedha kwa wakati  hivyo kukwami sha kazi hiyo.

Kwa upande wa  Katibu wa Makampuni ya Urasimishaji Ardhi Wilayani Ilala,  Clemence Mero, alisema changamoto kubwa ni wananchi kuto kulipa fedha, hivyo kampuni nyingi kushindwa kutekeleza wajibu kwa wakati.

“Kwa kweli hali hii imeshusha hata heshima ya kampuni zetu kwa kuitwa matapeli. Wananchi hawatoi fedha za kupiwa ardhi kiasi kwamba tunalazimika kutumia fedha zetu za mifukoni,”alisema.

Kwa upande wa wenye viti wa kamati za urasimishaji ardhi  wilayani humo, walisema kila sehemu  linapofanyika zoezi hilo kuna vilio vya wananchi kutapeliwa fedha na  kampuni husika.

“Hali ni mbaya. Tunaiomba serikali iingilie kati suala hili la urasimishaji. Wananchi hawatuamini tena  wenye viti wa kamati. Tunaonekana matapeli. Wamiliki wa kmpuniza urasimishaji hawapokei simu, hawahudhurii vikao na wengine wamefunga ofisi zao na kukimbia,” Alisema Bw George Mtambalike,