ACT-WAZLEZNDO: SERIKALI ICHUKUE HATUA KUDHIBITI KUPANDA BEI ZA BIDHAA MUHIMU
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Ado Shaibu akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.
CHAMA cha ACT-Wzalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua muafaka kuhakikisha kuwa bei za bidhaa muhimu inadhibitiwa ili kuwanusuru Watanzania wa chini.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 7, 2022 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari kuhuzu hoja tano za Wananchi katika ziara ya Sekretarieti ya ACT-Wazalendo Jimbo la Mbagala.
Licha ya jitihada ambazo Serikali inazichukua katika kuimarisha demokrasia, ni dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa kukabiliana na hali ngumu ya maisha ya Wananchi hazitoshi ikiwemo hoja ya kwanza ya kupanda kwa gharama za maisha na hali ngumu ya kiuchumi.
“Kote tulikopita, kilio kikubwa cha Wananchi ni hali ngumu ya maisha kunakotokana hasa na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama vile bidhaa za chakula, mafuta ya petroli na dizeli, bidhaa za ujenzi na nauli za usafiri wa daladala na za kwenda mikoani,” amesema Shaibu na kuongeza kwamba,
“Licha ya jitihada ambazo Serikali inazichukua katika kuimarisha demokrasia, ni dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa kukabiliana na hali ngumu ya maisha ya Wananchi hazitoshi. Serikali inapaswa kuchukua hatua muafaka kuhakikisha kuwa bei ya bidhaa muhimu inadhibitiwa ili kuwanusuru Watanzania wa chini,”.
Kwamba uchambuzi wa bei ya vyakula muhimu kama vile mchele, unga wa mahindi, mafuta ya kupikia na maharage imepanda sana ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka jana.
Ametolea mfano kuwa mchele umepanda kutoka Sh. 1,200 hadi 2,400, unga wa mahindi kutoka Sh. 1,000 hadi 1,600, mafuta ya kupikia kutoka Sh. 3,000 hadi 9,000, unga wa ngano kutoka Sh. 1,200 hadi 2,000, Sukari kutoka Sh. 1,500 hadi 3,000 na Nyama kutoka Sh. 6,500 hadi 9,000.l
Ameeleza kuwa, licha ya Serikali kutangaza kuingiza Sh. Bilioni 100 kama ruzuku kwenye ununuzi wa mafuta ili kupunguza bei, kwenye vituo vya mafuta Mbagala na kwingineko nchini bei ya mafuta inazidi kupaa, mathalani, bei ya mafuta ya petrol imepanda kutoka sh. 3,100 mwezi uliopita hadi sh. 3,220 mwezi huu.
“ACT Wazalendo tunarejea ushauri wetu uliotolewa na Msemaji wa Sekta ya Nishati Ndugu Isihaka Mchinjita kuishauri Serikali kuondosha sh. 500 kwa kila lita zinazokusanywa kama tozo ambapo itahakikisha kuwa Serikali inaweka ruzuku ya sh. bilioni 152.5 kila mwezi badala ya bilioni 100. Aidha, tunasisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwa kuyawezesha mashirika ya TIPER na TPDC kuagiza mafuta ili kuhakikisha unafuu zaidi unapatikana,” ameeleza Shaibu na kuongeza,
“Vile vile, Serikali itenge fedha haraka kwa ajili ya kuongeza uwezo wa hifadhi ya mafuta ya petroli ambapo itaongeza siku zaidi tofauti na utaratibu wa sasa wa kuagiza kila mwezi. Kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli ndiko kunakochochea kwa sehemu kubwa kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na nauli,”.
Ametaja hoja nyingine kuwa ni janga la ajira na changamoto mahsusi za Wamachinga, Bodaboda na Wafanyabiashara wa masokoni.
Kwamba kwenye Kata zote walizopita, Wananchi wanalia juu ya changamoto ya ajira ambapo vijana wasomi wanaendelea kumiminika mitaani huku uchumi wetu ukiwa hauzalishi fursa za kutosha kuwawezesha wahitimu wote kuajiliwa na kujiajiri.
Amsema mbali na hayo, vijana waliojiajiri kwenye sekta za bodaboda, wamachinga na wafanyabiashara masokoni, sekta ambazo zimeajiri vijana wengi, wamewaeleza kuwa Serikali haijaweka mazingira rafiki kwa wao kufanya shughuli zao.
“Mathalani, Wamachinga wa maeneo ya Mbagala Rangi Tatu wametueleza kuwa Serikali inawashinikiza kuondoka kuhamia maeneo ya Soko la Kampochea, Soko la Kijichi na Soko la Kilamba ambako kimsingi hakuna wateja wala mazingira rafiki ya kufanya biashara. Wengi, kwa kuinusuru mitaji yao, wamerejea tena Rangi Tatu kuendelea na biashara,” ameeleza na kusema,
“ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kufikiria upya mpango wake wa kuwapanga Wamachinga. Ni muhimu kuja na Mpango shirikishi ambao utazingatia maslahi mapana ya Wamachinga kufanya biashara kwenye maeneo yenye mzunguko mkubwa wa Biashara. Machinga ni Watanzania wanaotegemewa na familia zao. Shughuli zao za kujitafutia kipato zithaminiwe badala ya kuonekana watu wasiostahili kuwepo,”.
Akizungumza kwa upande wa Bodaboda na Bajaji, amesema wamewaeleza changamoto za bei ya mafuta, abiria kushindwa kumudu nauli halisi kutokana na ugumu wa maisha, kusumbuliwa na askari, hali duni ya usalama hasa wakati wa usiku na kuzuiliwa kuingia maeneo ya mjini.
Hivyo ameitaka Serikali ichukue hatua kuboresha mazingira ya bodaboda kufanya kazi ikiwemo kuwaruhusu kuingia mjini, kupunguza bei ya mafuta na kuwa na mkakati shirikishi wa kuhakikisha wanafuata sheria badala ya mahusiano ya "paka na panya" yaliyopo sasa baina yao na Askari wa Usalama Barabarani.
Ameongeza kwa upande wa masoko, Serikali ichukue hatua kuimarisha miundombinu ya masoko na ujenzi wa masoko uzingatie pia maoni ya wafanyabiashara ili kuepusha ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi ya masoko.
“Kwa mfano, Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonesha kuwa sehemu kubwa ya soko la Kijichi lililogharimu sh 765.1 milioni halitumiki kwa sababu ujenzi wake haukuzingatia mahitaji wa wafanyabiashara. Pia, ujenzi wa soko la Zakhem uliyeyuka licha ya kutengewa fedha sh. 2.26 bilioni,”.
Hoja nyongine amesema ni miundombinu mibovu na huduma duni za kijamii, Demokrasia, Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya na Uwajibikaji wa Serikali za Mitaa.
Shaibu ameeleza kutokana na uzoefu wa ziara ya Mbagala, Ofisi ya Katibu Mkuu itatoa Mwongozo Maalum kwa viongozi wa mikoa na majimbo kwa ajili ya kuzisemea changamoto za maeneo yao kwamba viongozi wa kila eneo watapimwa kwa namna wanavyozisemea changamoto za maeneo yao na kufanya uchambuzi wa kero za Wananchi.
Ameeleza kuwa viongozi watapaswa kutumia Taarifa za Kamati ya kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta kuiwajibisha Serikali kwenye maeneo yao.
Vile vile amesema chama kitazindua hivi karibuni, kupitia Halmashauri Kuu ya Chama Taifa, Sera ya Chama ya Wamachinga ambapo ameeleza kwenye Sera hiyo, wataweka bayana hatua ambazo Serikali inapaswa kuzichukua kuhakikisha kuwa Wamachinga wanafanya Shughuli zao kwa uhuru.
Aidha amebainisha kwamba kongamano la Kitaifa la Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya, ACT Wazalendo itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya kwa njia mbalimbali ikiwemo kufanya Makongamano ya Kitaifa ya Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya.
“Ninayo furaha kutangazia umma kuwa Kongamano la Nne la Kitaifa la Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya litafanyika Mkoani Tanga (Tanga Mjini) tarehe 23 Julai 2022. Kama ilivyo ada, Kongamano litawaleta pamoja viongozi, Wanachama na Wapenzi wa ACT Wazalendo kutathmini na kutoa mwelekeo wa ajenda ya mabadiliko kwenye eneo la Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya kwa kuzingatia hoja za ACT Wazalendo,”.




