Breaking News

MAJALIWA AVINYOSHEA KIDOLE VYOMBO VYA HABARI VYA NJE SAKATA LA NGORONGORO

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Viongozi wa Dini kuwa zoezi linaloendelea kwa wanaoama kutoka maeneo ya Ngorongoro linaendeshwa kwa utulivu na amani ambapo amedai kuwa Serikali imefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi wa jamii ya kimasai kupitia makundi mbalimbali pamoja na vyombo vya habari, huku akidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya nje Nchi vimekuwa vikiripoti sakata hilo katika namna hisiyo na dhamira njema.

Akizungumza leo Julai 10, 2022 wakati wa Sala na Baraza la Eid Al Adh'haa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Samia amesema amewahakishia viongozi wa Dini kuwa Nchi ya Tanzania ina amani na utulivu na kuwa katika sakata la Ngorongoro ambalo limeendelea kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii Serikali inalitekeleza zoezi la watu kuama kwa hiari na kuwa wametoa elimu kwa makundi tofauti pamoja na vyombo vya habari, lakini amedai kuwa baadhi ya vyombo vya habari kutoka nje ya Nchi ndivyo vimekuwa  vikiripoti sakata hilo kwa dhamira ambayo sio njema.

"Kwahiyo viongozi wa Dini tulisema namimi naomba nidokeze hili kwamba alichosema Mufti kwamba Nchi yetu ni salama na inaitaji kuwa salama na amani, nataka niwahakikishie Serikali katika hili tunatekeleza kwa amani, utulivu, mshikamano mzuri, tumetoa elimu kwa makundi, vyombo vya habari vimesaidia kutoa elimu hii, vinavyoangaika kutuaribia sisi ni vyombo vya nje vingine tu na sio hawa watu wetu, sikilizeni Serikali yenyu inasema nini katika hili"amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa 

Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo thabiti kuhusu sakata hilo ambayo ameeleza kuwa Serikali inayatekeleza maelekezo kwa ufasaha na kuwa  watamaliza zoezi hilo vizuri, na ametaka baadhi watu kuelewa dhamira ya Serikali kuwa wanalinda  rasilimali na tunu za Taifa huku akidai kuwa maeneo hayo yanayo hadhi na heshima kwa Taifa.

Majaliwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inapanga kuandaa utaratabu kwa viongozi wa Dini kwenda kutembelea maeneo Ngorongoro na eneo la  Msomera ambako amedai kuwa watu wanaamia kwa hiari 

"Nataka niwahakikishie viongozi Dini, na bado nina nafasi Wizara ya Maliasili na utalii tumeiagiza itengeneze utaratabu wa viongozi wa Dini tuwapeleke Msomera  hapa Tanga na tuwapeleke Ngorongoro mkiwa huko mtaona mazingira tuliyoyajenga mtazungumza na walioamia na kule Ngorongoro mtazungumza na wananchi muwaulize kwamba kuna mtu kapigwa, kuna mtu kalazimishwa"amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

"Lakini tuwapeleke kule porini kabisa mtusamehe tutawapeleka porini kwenye milima ambapo hakuna mtu hakuna nyumba lakini tutakwenda na nyie ili muone umbali kutoka vijiji mpaka huko kama kuna umuhimu wa kupeleka malundo ya ng'ombe uko ndani  harafu muone vyanzo ambavyo tukiruhusu Ng'ombe wakipelekwa wataviua harafu tuipoteze Serengeti mnayoijua ili na nyie mpate kujua." amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa 

Itakumbukwa sakata la Ngorongoro limekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii na kupelekea kuwepo kwa mitazamo kindhani juu ya sakata zima linaloendelea eneo la Tarafa ya Loliondo na Ngorongoro, ambapo baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakiripoti baadhi ya madai ya vitendo ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo vipigo na kumjeruhiwa kwa baadhi ya watu, lakini kauli ya Serikali imekuwa tofauti na madai hayo ambapo baadhi ya viongozi wa ngazi tofauti za Serikali wamekuwa wakidai kuwa zoezi hilo linaetekezwa kwa hiari na amani na utulivu huku wakisisitiza Wananchi kupuuza taarifa wanzodai kuwa ni zaupotoshaji.