Breaking News

WAZIRI UMMY: BADO HAKUNA MGONJWA WA HOMA YA MGUNDA

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema taarifa za ufuatiliaji wa ugonjwa wa homa ya mgunda (Leptospirosis) kutoka kwa wataalam walioko mkoani Lindi zinaonesha kuwa toka Julai 18, 2022 hadi sasa hakujawa na mgonjwa mpya aliyeonesha dalili za ugonjwa huu.

Waziri Ummy akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ugonjwa huo ambao Julai 18 mwaka huu ulitolewa taarifa kwa umma juu ya uwepo wake nchini baada ya uthibitisho wa kimaabara.

“Taarifa za ufuatiliaji wa ugonjwa huu kutoka kwa wataalam wetu walioko Mkoani Lindi zinaonesha kuwa toka tarehe 18 Julai 2022 hadi sasa hakujawa na mgonjwa mpya aliyeonesha dalili za ugonjwa huu. Hivyo hadi kufikia asubuhi ya leo tarehe 29 Julai 2022, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuugua ugonjwa huu nchini ni 20 na na kati yao 3 wamefariki,” amesema Waziri Ummy na kuongeza,

“Hivi sasa hakuna mgonjwa aliyelazwa wote wameruhusiwa kurudi nyumbani na wanaendelea na shughuli zao. Hii inaendana na sayansi inayojulikana kwa ugonjwa huu kuwa, ugonjwa huu unatibika kwa kutumia dawa ambazo zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini,”.

Aidha, amesema timu ya ufuatiliaji imebaini kuwa, miongoni mwa watu waliotangamana na wagonjwa hao (contacts) hakuna aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu hadi kufikia sasa.

Kwamba hiyo inadhihirisha pia, ni mara chache ugonjwa huu huambikizwa kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine, Vilevile, wataalamu wanaendelea na utafiti wa kina kwa binadamu, wanyama na mazingira yanayowazunguka ili kubaini na kuweka mikakati ya kuudhibiti ugonjwa huu nchini.

“Maandiko ya kisayansi yanaeleza kuwa, kwa kawaida ugonjwa huu unakuwa na dalili ambazo sio kali kwa asilimia 90, isipokuwa kwa wagonjwa wachache, (asilimia 10), wanaweza kuwa na dalili kali kama kutokwa na damu na kuathirika kwa viungo kama figo, ini n.k. Aidha, uwezo wa kuuchunguza kwa njia ya maabara upo hapa nchini, hivyo wananchi wanatakiwa kutokuwa na hofu. Ni muhimu wanapokuwa na dalili za ugonjwa huu kuwahi kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata matibabu stahiki na kwa wakati,” ameongeza Waziri Ummy.

Waziri Ummy amekumbusha kuwa ugonjwa wa homa ya Mgunda (leptospirosis) huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi.

Ameeleza, maambukizi ya ugonjwa huu kwenda kwa binadamu hupitia njiaza kugusa mkojo (au maji maji mengine ya mwili) kutoka kwa wanyama wenye maambukizi, kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi na kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo.

Vile vile amesema, bakteria wanaweza pia kuingia mwilini kupitia ngozi au utando wa macho, pua au mdomo (mucous membrane) na kupitia ngozi yenye mikwaruzo kwamba maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra sana.

“Wizara inaendelea kusisitiza kuwa, wananchi waendelee kuchukua tahadhari zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo kuepuka kutumia maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama pia kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa au kutibiwa,” amesema

Amewataka wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo ikiwemo homa, kuumuva kichwa, maumivu ya misuli, uchovu wa mwili, mwili kuwa na rangi ya manjano, macho kuvilia damu, kutoka damu puani, kukohoa damu, kichefuchefu na kuharisha kuhakikisha wanafika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mapema ili wapate uchunguzi na matibabu sahihi.