Breaking News

WIZARA YAKUTANA NA WADAU KUFANYA MAPITIO YA MKAKATI WA KITAIFA WA KUPAMBANA NA UJANGILI.

Katika kuendeleza mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii imekutana na wadau mbalimbali jijini Arusha ili kufanya  mapitio ya Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya Wanyamapori wa mwaka 2014 -2019.

Akifungua kikao kazi hicho kilichohusisha wadau kutoka taasisi za Wizara za Uhifadhi, baadhi ya wawakilishi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja Mataifa (UNDP)  na wadau kutoka Sekta binafsi, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Maurus Msuha amesema kikao kazi hicho kimeitishwa mahsusi kwa ajili ya kupitia mkakati uliopo kwa lengo la kuuhuisha ili uweze kwenda na wakati na kukidhi mahitaji ya sasa.

"Kazi ya uhifadhi ni ngumu, hili ndilo jukumu letu kuu katika Wizara. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilikuja na Mkakati wa miaka 5 wa kukabiliana na kupambana na ujangili na leo tumekutana ili kuhakikisha wadau wanapata fursa ya kufanya mapitio ya mkakati uliopo kwa lengo la kuuhuisha" 

Kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na juhudi za kudhibiti ujangili, Dkt. Msuha amesema  yametokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuanzishwa kwa Kikosi Kazi cha kupambana na ujangili, kuanzishwa kwa mifumo madhubuti ya kukabiliana na ujangili, mafunzo na uwezeshaji wa watumishi, kuzinduliwa kwa  mwongozo wa kuendesha mashtaka na ununuzi wa vitendea kazi.

Sababu nyingine ni kuimarika kwa ulinzi na usalama katika maeneo ya hifadhi, kukamatwa kwa silaha na majangili waliokua wakijihusisha na biashara  haramu na mitandao ya ujangili pamoja na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine katika mapambano dhidi ya ujangili.