CUF YAJIPANGA KUANZA KUDAI KATIBA MPYA NA TUME HURU YA UCHAGUZI
Dar es Salaam.
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kinatarajia kufanya mazungumzo na vyama vingine vya siasa kuhusu suala la Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Uamuzi huo wa CUF umechochewa na madai kwamba miswada iliyopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais kuwa sheria, ni danganya toto kwa kuwa maoni ya wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa siasa yalipuuzwa.
Februari 2024, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha miswada mitatu ambayo ni Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa.




