WADAU WA MAZAO YA MISITU NA NYUKI WAPONGEZWA USHIRIKI WAO MAONESHO YA NANENANE
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amewapongeza wadau wa mazao ya misitu na nyuki kwa kujitoleza kwenye mapnesho ya nanenane kutangaza bidhaa zao.
Naibu Waziri ameyasema hayo leo Agosti 7, 2024 alipokuwa anatembelea mabanda yaliyopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa Jijini Dodoma.
Amesema maonesho hayo ni fursa kwa wadau mbalimbali kutangaza fursa zitokanazo na mazao ya misitu ikiwemo mbao, mazao ya nyuki kama asali na mengine ili kupata masoko ndani na nje ya nchi.
"Maonesho haya yanakuwa na washiriki na wageni mbalimbali wanaotembelea mabanda kwaajili ya kuona bidhaa kutoka mataifa tofauti.
"Ni wakati sasa kuhakikisha bidhaa zinazotengenezwa na mazao ya misitu na nyuki zinatengenezwa kwa ubora mzuri ili kuwa na soko zuri la ndani na nje ya nchi" anasema.
Aidha, amepongeza juhudi za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao ya misitu na nyuki na kusisitiza bidhaa hizo kufungashwa vizuri na kwa ubora zaidi na kutangazwa ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa masoko ya bidhaa hizo.
Hata hivyo amesisitiza kutumia taarifa zinazopatikana kupitia mfumo wa satelite kuhusu utambuzi wa matukio ya moto kwa kutoa taarifa mapema katika eneo ambalo moto unaonekana umetoa ili kuondokana na madhara makubwa ambayo yamekuwa yakijitokeza katika misitu.
Naibu Waziri huyo aliyembelea maeneo mbalimbali yanayosimamiwa na Wizara ikiwepo sehemu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ikiwemo bustani ya miche ya miti ya kupanda na matunda, vivutio vya malikale na utalii ikolojia, wadau wa mazao ya misitu na nyuki ,shamba la nyuki na sehemu ya elimu ya utambuzi wa matukio ya moto kwa njia ya Satelite.
Viongozi na wananchi mbalimbali wanaendelea kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya Nanenane ambayo yalianza tangu terehe 1 Agosti 2024 ili kuona bidhaa na fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya Maliasili na Utalii.










